http://www.swahilihub.com/image/view/-/4927612/medRes/2219472/-/73t0b2z/-/karua.jpg

 

Karua: Serikali ikosolewe ila kwa njia ya heshima

Kiongozi wa Narc Kenya, Martha Karua  

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Wednesday, January 9  2019 at  13:58

Kwa Muhtasari

Watu hutofautiana kimawazo, japo huwa hawakoseani heshima wanapokosoana.


 

Nairobi, Kenya. Kiongozi wa Narc Kenya, Martha Karua amewahimiza wabunge wanaodai Rais Uhuru Kenyatta amepuuza kufanya maendeleo eneo la Mlima Kenya wamkosoe ipasavyo ila si kwa njia ya kumkosea heshima.

Karua amesema maendeleo huwa hayaishi, na ikiwa viongozi wanahisi maeneo wanayotoka yametelekezwa kuna njia bora za kuikosoa serikali.

"Lazima kiongozi wa taifa aheshimiwe, simaanishi serikali isikosolewe lakini kwa njia ya heshima," alisema waziri huyu wa zamani wa masuala ya haki mapema Jumatano. Aliongeza kusema kuwa watu hutofautiana kimawazo, japo huwa hawakoseani heshima wanapokosoana.

Kauli yake inajiri wakati ambapo malumbano yanaonekana kushika kasi katika mrengo tawala wa Jubilee unaoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake Dkt William Ruto, kufuatia madai ya mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria na mwenzake wa Bahati, Kimani Ngunjiri kuwa Rais amepuuza eneo la Kati kimaendeleo. Wakati wa mkesha wa kuukaribisha mwaka wa 2019, Kuria alisema Kenyatta anaendelea kuzindua miradi ya maendeleo maeneo ya upinzani akitelekeza alikotoka na ambako alichaguliwa kwa wingi.

Licha ya mbunge huyo kuomba kiongozi wa taifa msamaha kutokana na matamshi yake yanayochukuliwa kama ya kumkosea heshima, ameshikilia wakazi wa Mlima Kenya wameghadhabishwa na hatua ya Rais Kenyatta kufanya maendeleo ngome za upinzani huku akipuuza jamii yake. Kulingana na Karua ambaye mwaka uliopita aliwania ugavana Kirinyaga japo akabwagwa na Anne Mumbi Waiguru wa Jubilee, ni kwamba katika serikali za marais wastaafu, Daniel Moi na Mwai Kibaki, zilikosolewa zilipoenda mrama lakini si kwa kuwakosea heshima.

Akizungumza jijini Nairobi, wakili huyu alisema taswira inayooneshwa na wabunge hao kwa kizazi kijacho ni ya kupotosha akionya huenda wakaiga nyayo zao. Mnamo Jumatatu Rais Kenyatta akihutubu katika kaunti ya Mombasa wakati akizindua upya ukarabati wa bustani ya Mama Ngina, alisema maendeleo hayatafanywa kwa msingi wa anakotoka kiongozi na kuwa ni 'wetu'.

Akionekana kughadhabishwa na matamshi ya Kuria, Rais alisema atafanya maendeleo katika kila kona ya nchi huku akiwataka wanaomkosoa kukoma, "kwa hivyo hawa washenzi waachane na mimi". Baadhi ya viongozi na wanasiasa wa chama cha Jubilee pia wamemkashifu Kuria.

Hata hivyo, Karua ambaye 2013 aliwania kiti cha urais, anamsihi Rais Kenyatta kukaza kamba vita dhidi ya ufisadi akisema ndio umelemaza juhudi za maendeleo. Pia, amewataka wabunge kumuunga mkono Kenyatta katika jitihada hizo.