http://www.swahilihub.com/image/view/-/4927518/medRes/2219397/-/10bffql/-/seneti.jpg

 

Kauli ya Kipchumba Murkomen kuhusu msukosuko Jubilee

Kiongozi wa wengi,  Kipchumba Murkomen  

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Wednesday, January 9  2019 at  12:59

Kwa Muhtasari

Jubilee haiwezi ikasambaratishwa na Handshake

 

Nairobi, Kenya. Desemba 2018, Bw Murathe alisema jamii ya Mlima Kenya haina deni lolote kwa Naibu wa Rais William Ruto kuhusiana na siasa za urithi 2022. Alisema ikiwa Rais Kenyatta alikuwa ameahidi Naibu Rais jambo kama hilo, ni suala lao binafsi ila halihusishi jamii ya Mlima Kenya.

Kwa mujibu wa mkataba wa JP 2013, Dkt Ruto anapaswa kuunga mkono Kenyatta kuwa rais kwa kipindi cha miaka 10 kisha naye Kenyatta 'arudishe mkono' kwa kumpendekeza awanie urais. Mnamo Jumapili akitangaza kujiuzulu kwake kama naibu mwenyekiti wa JP, Murathe alisema hakuna mkataba wa aina hiyo ulioafikiwa akiwataka walionao wauoneshe taifa.

Alisisitiza kuwa ataelekea katika mahakama ya juu zaidi kumzuia Dkt Ruto kurithi Rais Kenyatta 2022 pamoja na kutaka ufafanuzi wa katiba iwapo anapaswa kuwa rais baada ya kuhudumu kama naibu rais kwa kipindi cha miaka 10.

Licha ya chungu cha JP kuonesha dalili za mgawanyiko, kiongozi wa wengi seneti Kipchumba Murkomen ameshikilia Jubilee ingali imara na kwamba si lazima Rais Kenyatta aoneshe bayana atamuunga mkono naibu wake 2022 kumrithi.

Amesema lililoko kwa sasa ni kuimarisha JP, iwe na sura ya kitaifa na mrengo unaojumuisha kila Mkenya kupitia umoja na utangamano. "Si lazima rais amuidhinishe naibu wake moja kwa moja. Tunaunda mrengo utakaokuwa na wawaniaji wengine wa urais 2022, na mchujo ndio utaamua ingawa naibu rais ndiye anavuma kwa sasa," alisema Murkomen.

Akiongea jana jijini Nairobi, kiongozi huyu wa wengi bunge la seneti alisema shabaha ya Jubilee ni kushawishi wananchi wajiunge na mrengo huo kwa ajili ya umoja wa kitaifa badala ya kuwatimua. Akirejelea suala la Murathe kujiuzulu, Murkomen alisema ni jambo lililojadiliwa na Rais Kenyatta na naibu wake. "Alipojiuzulu alisema kulikuwa na mashauriano ya viongozi wetu wakuu, ni ishara kuwa Rais na Naibu wa Rais wanaabiri mtumbwi mmoja," alisema.

Murathe alisema hatua ya kutaka kumzuia Dkt Ruto kuwania urais ni yake binafsi, Murkomen akisema umoja walioonesha Kenyatta na Ruto katika mashauriano ya kujiuzulu kwake ndio ulimshinikiza kuwapongeza.

Wandani wa Naibu Rais wamekuwa wakinyooshea kidole cha lawama kiongozi wa ODM Raila Odinga kwa masaibu yanayokumba Jubilee hasa baada ya salamu za mariadhiano kati ya Rais na Raila za Machi 2018, maarufu Handshake. Wamekuwa wakidai salamu hizo za heri zinalenga kuzima ndoto ya Dkt Ruto kumrithi Rais Kenyatta.

Murkomen jana alipuuzilia mbali tetesi hizo, akisema Jubilee haiwezi ikasambaratishwa na Handshake. "Ninaunga mkono salamu hizo za maridhiano, tulichopinga ni jinsi zilitafsiriwa," alisema. Hata hivyo, alisema anamezea mate utangamano na uongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini, ODM kinachoongozwa na Raila ambaye pia ni kinara wa Nasa.

"Ninamezea mate uongozi wa ODM, ndio wako nyuma yetu lakini kuna masuala sisi kama JP tunafaa kuwaiga. Chama chao kimedumu kwa miaka 10 ilhali chetu miaka mitano pekee," alisema. Raila ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa zamani amekuwa akikosoa Naibu Rais kuwa anafanya siasa za 2022, akihoji anakiuka matakwa ya Handshake.