http://www.swahilihub.com/image/view/-/1619980/medRes/870564/-/51ektl/-/Kavuludi.jpg

 

Kavuludi aingilia kati mzozo wa nafasi za wakuu wa polisi

Johnstone Kavuludi.

Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Huduma za Polisi Johnstone Kavuludi. Picha/MARTIN MUKANGU 

Na VALENTINE OBARA

Imepakiwa - Thursday, January 11  2018 at  22:27

Kwa Muhtasari

MWENYEKITI wa Tume ya Kitaifa ya Huduma za Polisi (NPSC), Bw Johnston Kavuludi, ameingilia kati mzozo kuhusu uteuzi wa kaimu wakuu wa polisi nchini kwa kutangaza wazi nafasi hizo na kualika maombi kutoka kwa wanaozitaka.

 

Kinara wa Muungano wa NASA, Bw Raila Odinga, amepinga hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kuteua Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), Kaimu Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi wa Utawala na Kaimu Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi wa Kawaida.

Kulingana na Bw Odinga, rais alikiuka sheria kwa sababu jukumu hilo ni la tume ya NPSC. Bw Kavuludi Alhamisi alichapisha tangazo kutoa wito kwa Wakenya watume maombi kujaza nafasi hizo tatu.

“Kwa msingi wa katiba...Tume ya Kitaifa ya Huduma za Polisi inatazamia kuajiri manaibu inspekta jenerali na mkurugenzi wa idara ya upelelezi wa jinai ambao wanafikia mahitaji ya katiba,” ikasema sehemu ya tangazo hilo.

Wiki iliyopita, rais alitumia mamlaka yake ya kisheria kumuondoa aliyekuwa mkurugenizi wa DCI, Bw Ndegwa Muhoro, aliyekuwa Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi wa Kawaida, Bw Joel Kitili, na aliyekuwa Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi wa Utawala, Bw Samuel Arachi.

Mahali pao aliteua Bw George Kinoti, Bw Edward Mbugua na Bw Noor Gabow kushikilia nyadhifa hizo. Bw Odinga alipinga hatua hiyo akisema ilikiuka katiba na inatia hofu kizingatiwa jinsi polisi walivyohusishwa na ukatili mkubwa dhidi ya wakosoaji wake mwaka uliopita.

“Hili ni dhihirisho la kudunisha mamlaka za idara zinazofaa kuwa huru kwa nia ya kuimarisha utawala wa kiimla,” akasema Bw Odinga.

Mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu, Bw Ndung’u Wainaina, alidai rais alifanya uteuzi huo ili kushawishi uamuzi utakaofanywa na jopo la Bw Kavuludi.

“Huu ni mfano wa jinsi Rais Kenyatta anavyoingilia taasisi huru na kutoheshimu katiba,” akasema kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter Alhamisi.

Kulingana na sheria inayosimamia huduma za polisi, NPSC inahitajika kuwasilisha majina ya watu wanaopendekezwa kujaza nafasi hizo kwa rais wakati nafasi hizo zinapobaki wazi.

Rais atakuwa na siku 14 kuanzia siku ambayo nafasi hizo zilibaki wazi kuchagua anayefaa kuzijaza.

Katika tangazo lake, Bw Kavuludi alisema watu ambao wamewahi kuhukumiwa kwa aina yoyote ya uhalifu hawatakubaliwa kuomba nyadhifa hizo.

Wengine watakaokataliwa ni waliokiuka katiba kwa njia yoyote, waliofilisika, na waliotajwa sana katika upelelezi wowote wa tume za uchunguzi au kamati za Bunge.

Tume hiyo pia ilisema itamtupa nje mtu yeyote atakayetumia ushawishi wa aina yoyote kutafuta kazi hizo au atakayetoa habari za uongo kumhusu.