http://www.swahilihub.com/image/view/-/4842564/medRes/1154143/-/14y55j/-/DnMashujaaDay2010%25285%2529.jpg

 

Kenyatta asisitiza KDF kusalia Somalia mpaka kieleweke

Uhuru Kenyatta na Samson Mwathethe

Rais Uhuru Kenyatta azungumza na Mkuu wa Jeshi Jenerali Samson Mwathethe. Picha/MAKTABA 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Thursday, November 8  2018 at  13:59

Kwa Muhtasari

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesisitiza wanajeshi wa KDF hawataondoka Somalia mpaka wahakikishe magaidi wameisha si tu nchini Somalia na Kenya, lakini katika eneo zima la Afrika Mashariki.

 

ELDORET, Kenya

WANAJESHI wa Kenya (KDF) waliopo nchini Somalia watasalia nchini humo hadi pale magaidi watasalimu amri, amesema Rais Uhuru Kenyatta.

Kiongozi huyu wa taifa ameshikilia kwamba hawataondoka Somalia hadi wahakikishe magaidi wameisha si tu katika nchi ya Somalia na Kenya, ila katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Akihutubu Alhamisi katika hafla ya kufuzu kwa makurutu wa KDF katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Moi Barracks, Eldoret, Rais Kenyatta ameahidi kuwa serikali itaendelea kuunga mkono na kufadhili oparesheni inayoendeshwa na maafisa hao Somalia.

"Serikali inajali usalama wa raia wake, maafisa wetu wataendelea kusalia Somalia hadi magaidi wasalimu," amesema Rais. Kenyatta aidha, amewataka maafisa waliofuzu kuungana na maafisa wengine wa usalama katika vita dhidi ya magaidi nchini.

Zaidi ya makurutu 3,000 wamefuzu katika chuo hicho.

Maafisa wa KDF wamekuwa wakihudumu Somalia chini ya muungano wa kimisheni wa Amisom, unaojumuisha majeshi ya nchi kadha Afrika Mashariki, kutoka muungano wa Bara Afrika (AU) na Marekani.

Operesheni ya wanajeshi hao nchini humo ilianza Oktoba 2011, chini ya utawala wa Rais (mstaafu) Mwai Kibaki na kiongozi wa Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga wakati huo akiwa Waziri Mkuu.

Magaidi wa al-Shabaab

Amri ya Rais Kibaki kuwatuma humo ilitokana na ongezeko la mashambulizi ya kigaidi yaliyoendeshwa na kundi haramu la al-Shabaab nchini na mataifa mengine Afrika Mashariki.

Kuwepo kwa wanajeshi wa Kenya Somalia kumekuwa kukikosolewa na baadhi ya wanaharakati na hata viongozi. Maafisa kadha wameripotiwa kuuawa kwa kushambuliwa na magaidi.