http://www.swahilihub.com/image/view/-/2705554/medRes/1002202/-/v7v3pm/-/UhuruVideoAddress.jpg

 

Rais Kenyatta awataka mawaziri wake kuwajibika zaidi

Rais Uhuru Kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta akihutubu awali. Picha/PSCU  

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Friday, February 1  2019 at  10:53

Kwa Muhtasari

Kiongozi wa taifa la Kenya amewataka mawaziri wake kufanyia wananchi kazi badala ya kujihusisha sana na siasa; hasa za urais mwaka 2022.

 

KAJIADO, Kenya

MAWAZIRI wametakiwa kujiepusha kushiriki siasa na badala yake watekeleze majukumu waliyoteuliwa kufanya.

Rais Uhuru Kenyatta ameonya kuwa serikali yake, Jubilee, haina nafasi ya mawaziri wanaofanya siasa wakati inapambana kuafikia ahadi zake kwa wananchi.

Rais Kenyatta mnamo Alhamisi alilitaka baraza lake la mawaziri kukumbatia mfumo wa kuzuru mashinani na kujua shida wanazopitia wananchi ili serikali izitatue.

Akihutubia umati eneo la Kitengela, Kajiado, alisema maendeleo yatafanyika ikiwa viongozi waliokabidhiwa majukumu na serikali watatangamana na wananchi.

"Wewe ukishindwa na kazi, 'piga abautani'. Yetu sisi ni kazi, waje hapa Kitengela wawaulize taabu yenu ni ipi ili sirkali iwafanyie kazi si kuja hapa porojo na siasa," alionya Rais, akionekana kughadhbishwa na baadhi ya mawaziri ingawa hakuwataja.

"Kama siasa yako ni stori, enda kwingine serikali ya Uhuru Kenyatta itatimiza ahadi za watu wa Kenya," aliongeza.

Kiongozi wa taifa alikuwa ameandamana na naibu wake Dkt William Ruto, ambapo alikuwa akielekea mjini Arusha, Tanzania kwa kongamano la Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC.

Naibu wa Rais alitilia mkazo matamshi ya Kenyatta, akihimiza viongozi kuepuka kushiriki siasa.

"Rais amesema fitina kando siasa kando ufisadi nyuma, tusongeshe hii nchi mbele," akasema Dkt Ruto.

Matamshi ya Rais Kenyatta kwa mawaziri yamejiri siku chache baada ya kumteua Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang'i kama mwenyekiti wa kamati simamizi ya miradi yote ya serikali na mawaziri, wadhifa unaochukuliwa sawa na wa waziri mkuu au kwa kifupi ni waziri kinara.

Siasa za 2022

Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga wamekuwa katika mstari wa mbele kukashifu siasa za mapema za 2022.

Tangu viongozi hawa wawili wafanye salamu za maridhiano maarufu March Handshake, wamekuwa wakifanya misururu ya ziara sehemu mbalimbali nchini kwa msingi wa vigezo vya mkataba huo.