http://www.swahilihub.com/image/view/-/4217166/medRes/1829256/-/jrd7lrz/-/KIMUNYA.jpg

 

Kesi ya ulaghai wa shamba dhidi ya Kimunya yaahirishwa

Amos Kimunya

Aliyekuwa Waziri wa Fedha Amos Kimunya (kati) akiondoka mahakama ya Milimani Jumanne. Picha/RICHARD MUNGUTI 

Na  RICHARD MUNGUTI

Imepakiwa - Wednesday, December 6  2017 at  15:28

Kwa Muhtasari

MAHAKAMA inayoamua kesi za ufisadi Jumanne iliahirisha kesi ya ulaghai wa shamba dhidi ya aliyekuwa waziri wa fedha Amos Kimunya hadi Machi 2018.

 

Wakili wa Serikali Daniel Karori alimweleza hakimu mwandamizi Bw Felix Kombo kwamba anahutaji muda huo kuwafikia mashahidi.

Akiomba mahakama impe muda wa kuwafikia mashahidi ambao walitarajiwa kufika kortini kutoa ushahidi, kiongozi wa mashtaka Bw Daniel Karori alisema wamekubaliana na mawakili wanaowakilisha washukiwa kesi hiyo ianze kusikizwa Machi 12, 2018.

Hakimu mwandamizi Bw Felix Kombo anayesikiza kesi hiyo alimtaka  Bw Karuri atilie maanani kwamba kesi hiyo ilianza miaka mitatu iliyopita na  mwongozo wa Jaji Mkuu (CJ) Bw David Maraga ni kwamba, kesi zikamilishwe kusikizwa katika muda unaofaa.

Bw Kimunya ambaye aliwahi hudumu kama Waziri wa Fedha mwandamizi amekanusha mashtaka kwamba mnamo Juni 30, 2005 akiwa Waziri wa Ardhi na Nyumba,  alitumia mamlaka ya afisi yake vibaya na kusajili shamba la kupanda viazi la Serikali kwa kampuni ya kibinafsi.

Mahakama ilielezwa Bw Kimunya aliandikisha shamba hilo la umma kwa kampuni ijulikanayo kama Midlands Limited.

Shtaka hilo pia ladai Bw Kimunya alijua kwamba shamba hilo halikuwa la kuuzwa ama kubadilishwa umiliki.

Bw Kimunya pia anakabiliwa na mashtaka ya kuuza mali ya umma kinyume cha sheria.

Mahakama ilifahamishwa kwamba  waziri aliuzia kampuni yake ya Midland shamba hilo la umma.