http://www.swahilihub.com/image/view/-/3111106/medRes/727057/-/1r62op/-/DnEUTrip0104v.jpg

 

Karanja Kibicho asema wanaopanga kumwapisha Raila 'hamtutishi'

Karanja Kibicho

Dkt Karanja Kibicho. Picha/MAKTABA 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Tuesday, November 14  2017 at  06:59

Kwa Muhtasari

Katibu maalum katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Karanja Kibicho, alisema Jumatatu kuwa hadi sasa sheria za Kenya hazitambui kiapo cha Raila Odinga kuchukua majukumu ya urais; lakini pia ni mapema kuzima yeyote aliye na imani ya kumwapisha.

 

KATIBU maalum katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Karanja Kibicho, alisema Jumatatu kuwa hadi sasa sheria za Kenya hazitambui kiapo cha Raila Odinga kuchukua majukumu ya urais; lakini pia ni mapema kuzima yeyote aliye na imani ya kumwapisha.

Alisema kuwa serikali iliyo mamlakani kwa sasa imewezeshwa kikatiba kuzima harakati za kuhujumu katiba na ikiwa kutakuwa na jaribio la aina hiyo, basi washirikishi walo watakabiliwa kisheria "ingawa sasa hivi ni mapema mno".

Kibicho alikuwa akijibu swali la mtandao wa Swahilihub kuhusu nini Wakenya watategemea kutoka kwa serikali iwapo tishio la kisiasa kuwa kinara wa Nasa, ataapishwa sambamba na Rais Uhuru Kenyatta ikiwa kesi iliyo mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 26 yatatoa mwanya wa kuapishwa kwa Kenyatta.

Mrengo huo wa Nasa umeshikilia kuwa hautambui urais wa Kenyatta na ikiwa ataapishwa, basi naye Odinga ataapishwa katika hafla mbadala.

Kibicho alisema, “Hadi sasa tunachukulia mito hiyo kama ya kisiasa na ambapo hakuna uwezekano wowote wa kisheria wa hilo kufanyika. Lakini sio kumaanisha hatuchukulii jumbe hizo kwa uzito.”

Kibicho alisema kuwa kwa sasa hakuna ule msukumo mkubwa wa vitengo vya kiusalama kuwajibikia tishio hilo.

“Unajua kuwa hadi sasa tunangojea mahakama ya juu zaidi itoe mwelekeo wa kuapishwa kwa rais. Ikiwa kesi iliyo mahakamani ya kupinga ushindi wa rais Kenyatta itatupiliwa mbali, basi tutaingia katika awamu muhimu ya kuwa na uhakika kuhusu maandalizi ya hafla ya kumlisha kiapo,” akasema.

Alisema kuwa hafla hiyo huwa ni ya kitaifa na vitengo vyote vya kiusalama huwekwa chonjo kwa kuwa vina uhakika wa ni nani kiongozi wa taifa na aliye amiri mkuu wa majeshi.

“Hapo ndipo sasa tungetaka mrengo wa Nasa useme kwa uhakika kuwa unapanga kumwapisha raia ambaye hakuchaguliwa na watu na hajapewa ilani ya mahakama kuwa yeye ndiye anafaa kuapishwa. Hapo ndipo wanaosambaza jumbe za kiapo haramu watajua kuna sheria Kenya hii,” akasema.

Alisema kuwa kwa sasa kila mtu anaweza kuendelea mbele na kutangaza kuwa angetaka aapishwe kuwa rais lakini wakati mahakama ya juu itatoa mwelekeo wa uhakika wa ni nani anafaa kuapishwa, ndipo nitakutahadharisha uwe makini sana na unayotoa kwa mdomo wako.