http://www.swahilihub.com/image/view/-/4304054/medRes/1884463/-/sqc60qz/-/kariuki.jpg

 

Rais awasilisha bungeni jina la Paul Kihara Kariuki kuidhinishwa awe Mwanasheria Mkuu

Paul Kihara Kariuki

Mwanasheria mkuu Paul Kihara Kariuki aliyeteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta baada ya Profesa Githu Muigai kujiuzulu Februari 13, 2018. Picha/MAKTABA 

Na MWANDISHI WETU

Imepakiwa - Tuesday, March 13  2018 at  15:19

Kwa Muhtasari

Rais Uhuru Kenyatta amewasilisha jina la Kihara Kariuki kuidhinishwa katika bunge la kitaifa akipendekeza awe Mwanasheria Mkuu.

 

RAIS Uhuru Kenyatta amewasilisha jina la Kihara Kariuki kuidhinishwa katika bunge la kitaifa akipendekeza awe Mkuu wa Sheria.

Jaji Paul Kihara Kariuki aliyekuwa mkuu wa kitengo cha rufaa cha mahakama sasa ndiye anatazamiwa kutwaa majukumu ya mwanasheria mkuu hapa nchini.

Hii ni baada ya Rais Uhuru Kenyatta kumtaja kama aliyependekezwa kujaza nafasi hiyo baada ya kujizulu kwa Priof Githu Muigai hapo Jumanne.

Ingawa sio suala la kawaida kwa anayeshikilia wadhifa huo kujizulu pasipo na sababu nyeti, hivyo basi kuashiria Prof Muigai alisukumwa kufanya hivyo ili afisi hiyo itekelezewe mabadiliko, cha maana ni kuwa Jaji Kariuki ako langoni akibisha kuingia.

Akiidhinishwa na bunge la kitaifa, basi, kutakuwa na Mwanasheria Mkuu mpya.

Ni Jaji aliye na tajiriba ya juu na ueledi mkuu katika mahakama ambapo aliingia katika huduma ya uwakili hapa nchini mwaka wa 1978, Rais Kenyatta akiwa na miaka 14 pekee.

Asahawahi kuhudumu kama Kamishna wa baraza la Jiji la Nairobi kati ya 1985 na 1986 na akawajibishwa majukumu katika bodi ya kupambana na ufisadi hapa nchini kati ya 1997 na 1998.

Akifahamika na walio karibu naye kama anayependa kutangamana kimaisha na aliye na usiri mkuu kuhusu maisha yake ya kibinafsi, Jaji Kariuki ni mwanakamati katika Ushirika wa Mawajkili nchini, (LSK).

Na katika ile hali ambayo tayari imeanza kuzua cheche za malalamiko kuhusu serikali ya Rais Kenyatta kupanua shughuli zake za uvuvi ili kuwanasa wa kuteuliwa katika nyadhifa kuu serikalini, Jaji Kariuki ni mzawa wa Kaunti ya Kiambu.

Kiambu ikiwa ndiyo tu Kaunti ya kuzaliwa ya rais Kenyatta, Jaji Kariuki alizaliwa Mei 11, 1954, akiwa mwana wa Mzee Obadiah Kariuki na Mama Lilian Wairimu.

Ana shahada ya uwakili kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi ambayo alipata alipofuzu masomo mwaka wa 1977.

Alianza huduma yake ya uwakili katika kampuni ya Hamilton Harrison na Matthews iliyoko Jijini Nairobi akiwa msaidizi wa masuala ya kisheria na ambapo alihudumu kati ya 1977 na 1980.

Alikubalika kuwa mshirika ndani ya Kampuni hiyo mwaka wa 1981 hadi 1986 kabla ya kuhamia katika Kampuni ya uanasheria ya Ndungu Njoroge na Kwach kati ya 1986 na 2000.

Ni mwekezaji tajika ambapo ni mkurugenzi wa kampuni kadhaa ndani ya muungano wa International Controls; uwekezaji wa tangu mwaka wa 2000.

Mkristo, lakini aliye na uhuru wa kuhusika na moja mawili ya maisha ya kawaida katika faragha kimaisha hasa katika eneo la Rift Valley, alikuwa Chansela wa kanisa la Kianglikana kati ya 1980 hadi 2001 ikizingatiwa kuwa marehemu babake aliyezaliwa mwaka wa 1902 alikuwa mchungaji.

Anajifahamisha kama anayependa ubunifu wa sanaa na michezo kama Squash, Kriketi na pia masuala ya kilimo.

Maisha ya ndoa

Alimuoa Sarah Njoki Kimingi Kariuki mnamo Septemba 4, 1976, na kwa pamoja wamejaliwa watoto wanaotambulika kwa majina Marion Wairimu, Andrew Kariuki na Zazira Njeri.

Huku kukionekana kuwa na malumbano kati ya serikali ya Jubilee na idara ya mahakama kwa sasa na ambayo yanachangiwa pakubwa na mawimbi
ya kisiasa, Jaji Kariuki anatarajiwa kuwa kiungo muhimu katika kuleta ule uwiano na utulivu katika uhusiano wa idar6a hizo mbili muhimu za kiutawala.