Kimemia aahidi kufufua uchumi wa Nyandarua siku 100 za mwanzo

Francis Kimemia

Francis Kimemia akihutubu awali. Picha/BILLY MUTAI 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Saturday, August 12   2017 at  13:53

Kwa Mukhtasari

Gavana mpya wa Kaunti ya Nyandarua, Francis Thuita Kimemia amesema kuwa katika kipindi cha siku 100 zake afisini, atakuwa ameandaa ratiba thabiti ya kuelekeza Kaunti hiyo hadi uthabiti wa kiuchumi.

 

GAVANA mpya wa Kaunti ya Nyandarua, Francis Thuita Kimemia amesema kuwa katika kipindi cha siku 100 zake afisini, atakuwa ameandaa ratiba thabiti ya kuelekeza Kaunti hiyo hadi uthabiti wa kiuchumi.

Ameahidi kuwa sekta ya kilimo ndiyo kwa upana itatumika kuandaa mikakati hiyo ambapo “ni lazima mkulima wa Nyandarua alindwe dhidi ya
athari za biashara bovu.”

Amesema kuwa hadi sasa mkulima katika Kaunti hiyo hana la kujivunia katika utawala wa ugatuzi ambapo usimamizi wa sekta hiyo ya kilimo ulihamishwa hadi kwa uratibu wa serikali ya Kaunti.

“Kwa mfano, mkulima wa viazi hapa Nyandarua ameendelea kuathirika na utekaji nyara wa sekta hiyo na madalali. Madalali ambao hununua gunia
la kilo 200 la viazi kwa bei inayofaa gunia la kilo 50. Unapata kwamba pato la mkulima linaibiwa kwa kiwango cha asilimia 400,” amesema.

Amesema kuwa utawala wake utaweka sheria kuwa hakuna gunia la kilo 200 litakuwa linapakiwa viazi katika Kaunti hiyo.

Amesema kuwa utawala ambao ameutimua mamlakani kupitia ushindi wake wa kura ya Agosti 8 haukuwa na nia au uwezo kurekebisha hali hiyo.

“Ni kwa sababu utawala huo wa gavana Waithaka Mwangi haukutilia mkazo mashauriano kati ya raia na serikali yake. Angefanya hivyo, angekuwa
na uwezo wa kujua kero hilo dhidi ya wakulima wa Nyandarua na kisha asukume bunge lake la madiwani kutekeleza mikakati mwafaka ya kuokoa
wakulima hao,” amesema.

Amesema kuwa pesa za bajeti ambazo serikali hiyo imekuwa ikipokezwa na serikali kuu zilikuwa zikitumiwa visivyo.

"Miradi iliyogharimu pesa hizo kwa ukubwa ni ya njama za wizi na kujinufaisha pasipo kumjali mpiga kura wa Nyandarua na familia za Nyandarua,” amesema Kimemia.

Kimemia ameongeza kuwa ataandaa kongamano kadhaa za majadiliano ili kuibuka na ratiba mwafaka ya kushugulikia changamoto ambazo zinakumba
eneo hilo.

“Ni kupitia majadiliano ambapo tutapata shida za mkazi wa Nyandarua. Ni kupitia majadiliano hayo ambapo tutapata ratiba ya kuzishughulikia
changamoto hizo,” akasema.

Kimemia amesema kuwa amegundua watu wa Nyandarua ni werevu na wamemakinika kisiasa “kiasi cha kugundua utawala mbaya ambao hauwafai".

Amesema kuwa kwa kuwa hangetaka kujipata katika hali ya kutimuliwa mamlakani 2022, atajitahidi kuwatekelezea haki ya kiutawala watu wa
Nyandarua.