Kivumbi chatarajiwa kwenye mchujo wa Jubilee

Raphael Tuju

Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee Raphael Tuju akihutubia wanahabari. PICHA/ LEONARD ONYANGO 

Na BERNARDINE MUTANU

Imepakiwa - Thursday, April 20  2017 at  18:17

Kwa Mukhtasari

KIVUMBI kikubwa kinatarajiwa wakati wa shughuli ya mchujo ya Chama cha Jubilee inayotarajiwa kuanza Ijumaa Aprili 21.

 

Katika Kaunti ya Nairobi, kivumbi kinatarajiwa kati ya Seneta Gideon Mbuvi na Bw Peter Kenneth ambao wameonekana kutofautiana hasa baada ya habari kuibuka kwamba chama cha Jubilee kina baadhi ya wawaniaji ambao kinapendelea.

Mapema wiki hii, chama hicho kilituma taarifa kukana kwamba Rais Uhuru Kenyatta alikuwa amemwidhinisha Peter Kenneth kuwania wadhifa wa ugavana Nairobi kwa tiketi yake.

Katika Kaunti ya Uasin Gishu, tayari Gavana Jackson Mandago anahisi kutishiwa na Zedekiah Kiprop, kwa jina la msimbo, Buzeki, ambaye amefifisha matumaini yake ya kupata tiketi ya Jubilee.

Aidha, Mandago amemlaumu Naibu wa Rais William Ruto kwa kusema kuwa ameonekana kumpendelea Buzeki.

Katika Kaunti ya Kiambu, Gavana William Kabogo na Mbunge wa Kabete Ferdinand Waititu wanatarajiwa kuwa na ushindani mkali.

Hali inatarajiwa kuwa kama hiyo katika Kaunti ya Murang’a ambako Gavana Mwangi wa Iria anashindana na Mbunge wa Kigumo Jamleck Kamau.

Ushindani mkali unatarajiwa vile vile Embu ambako wadhifa wa ugavana umewavutia wawaniaji watatu, Gavana Martin Wambora, Seneta Lenny Kivuti na Mbunge wa Runyenjes, Cecily Mbarire.

Katika Kaunti ya Nakuru, ushindani mkali unatarajiwa kati ya Gavana Kinuthia Mbugua, Lee Kinyanjui na Bw John Mututho.

Hali haitakuwa tofauti katika Kaunti ya Laikipia ambako wawaniaji watatu wanamezea mate tiketi ya Jubilee kuwania ugavana.

Wawaniaji hao ni Gavana Joshua Irungu, mpwawe aliyekuwa rais Ndiritu Muriithi na aliyekuwa Katibu Mkuu katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni,Thuita Mwangi.

Tayari, machafuko yameshuhudiwa katika maeneo kadhaa nchini, ambako Jubilee ina ufuasi mkubwa.

Bw Musangi alisema muda wa utekelezaji wa shughuli umerefushwa kutokana na kuwa kaunti ambako Jubilee inatekeleza uteuzi wake zimeongezeka kutoka kaunti 33 hadi kaunti 45.

Licha ya kurefusha muda wa mchujo, Bw Musangi alisema idadi ya wawaniaji watakaoshiriki katika shughuli hiyo hajaongezeka na itasalia kadiri ya 8,000.

Kulingana na NEB, maafisa watakaofanyisha mchujo huo watabadilishwa ili wasihudumu katika maeneo wanayotoka, kuhakikisha uchaguzi huru na haki, alisema mwenyekiti huyo.