http://www.swahilihub.com/image/view/-/4345306/medRes/1911086/-/10fnffuz/-/geda.jpg

 

Gavana Laboso aadhimisha mwaka mmoja ofisini kwa kuahidi mengi mazuri

Dkt Joyce Laboso

Gavana wa Bomet Dkt Joyce Laboso azindua ujenzi wa barabara za kilomita 150 katika kaunti hiyo Februari 20, 2018. Picha/BENSON MOMANYI 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Friday, September 14  2018 at  13:35

Kwa Muhtasari

Kaunti ya Bomet inaadhimisha mwaka mmoja tangu Joyce Laboso achaguliwe gavana wake Agosti 2017.

 

BOMET, Kenya

KAUNTI ya Bomet leo Ijumaa inaadhimisha mwaka mmoja tangu Joyce Laboso achaguliwe gavana wake Agosti 2017.

Bi Joyce Cherono Laboso aliyewania wadhifa huo kwa tiketi ya chama tawala cha Jubilee, alizoa kura 175,932 dhidi ya mpinzani wake Isaac Rutto wa Chama Cha Mashinani (CCM) aliyepata 85863.

Rutto ndiye alikuwa gavana wa Bomet tangu mwaka 2013.

Hafla hiyo imeandaliwa katika uwanja wa Bomet Green Stadium, na Laboso amesema inalenga kuleta pamoja wakazi wa kaunti hiyo.

"Sherehe hii mwanzo ni ya kumshukuru Mungu, ambapo wakazi wa Bomet watakuja pamoja," gavana huyo akaambia waandishi wa habari katika uwanja huo, ambao ni wa tatu kwa ukubwa nchini Kenya.

Laboso ameongeza kuwa atatumia jukwaa hilo kueleza wakazi wa Bomet miradi ya maendeleo ambayo serikali yake imefanya kwa muda wa mwaka mmoja ofisini.

"Serikali yangu imeweka lami barabara yenye urefu wa kilomita 400, kuongeza shule za chekechea ikiwa ni pamoja na kuimarisha kilimo cha majani ya chai," akaeleza gavana huyo.

Siasa

Hata hivyo, amewataka wakazi wa kaunti yake kujiepusha na siasa za kuhujumu ajenda zake akisema kipindi cha siasa kiliisha 2017 na kwamba huu ni wakati wa kuchapa kazi.

Joto la kisiasa Bomet mwaka jana lilikuwa limepanda kwa sababu ya ushindani wake na Rutto, lakini Laboso anajipigia debe akisema amefanikiwa kuliondoa "kwa kuwa yeye ni mama anayeelewa masaibu ya familia yake".