Madiwani waliomzuia mwalimu mkuu Kibwezi wakamatwa

Na PIUS MAUNDU na CHARLES WASONGA

Imepakiwa - Thursday, January 11  2018 at  21:34

Kwa Mukhtasari

POLISI Alhamisi waliwakamata madiwani sita wa kaunti ya Makueni ambao walijaribu kuzuia mwalimu mkuu mpya kushika usukani katika Shule ya Upili ya Wasichana ya St Josephs, Kibwezi.

 

Sita hao walizuiliwa katika kituo cha polisi wakisubiri kuwasilishwa mahakamani Ijumaa, Kamishna wa kaunti hiyo Mohammed Maalim alithibitisha.

"Hatutasema ni wapi au lini watapelekwa kortini, lakini nathibitisha kuwa watapelekwa kortini kufunguliwa mashtaka baada ya muda usiokuwa mrefu," Bw Maalim akaambia SwahiliHub kwa njia ya simu.

Wanasiasa hao walikamatwa wakati walipokuwa wameketi katika mkutano na maafisa wa elimu wa kaunti ya Makueni na wanachama wa bodi ya usimamizi wa shule hiyo mwendo wa saa tisa alasiri. Walipelekwa hadi mjini Mtito Andei, ulioko umbali wa kilomita 40, na kufungiwa katika kituo cha polisi.

Wakiongozwa na Diwani wa wadi ya Thange Nicholas Maitha ambye ni mwenyekiti wa kamati ya Elimu katika Bunge la Kaunti ya Makueni, madiwani hao awali walikabiliana na polisi na maafisa wa elimu wakijaribu kuzuia Bi Rose Kiragu kuanza kazi kama Mwalimu Mkuu mpya wa shule hiyo.

Walipinga kile walichodai ni "kulazimishwa" kwa Bi Kiragu katika shule hiyo ya ngazi ya kaunti. Wakiunga mkono msimamo wa bodi ya usimamizi wa shule hiyo wiki iliyopita wa kumtaka mwalimu mkuu huyo, wanasiasa hao walidaiwa kuwa Bi Kiragu anakabiliwa na kesi za utovu wa nidhamu katika shule yake ya zamani na wakaapa kutomruhusu kusimamia shule hiyo 

Vile vile, inadaiwa kuwa Mwalimu Mkuu huyo haelewani na Kanisa Katoliki ambalo husimamia shule hiyo ya upili ya wasichana. Juhudi zetu za kuthibitisha madai dhidi ya Bi Kiragu, hata hivyo, ziligonga mwamba.

Awali fujo zilitokea katika lango kuu la shule hiyo pale madiwani hao na maafisa wa elimu waliporushiana cheche za maneno kabla ya polisi wa kupambana na ghasia kuwasili na kuingilia kati.

Maafisa hao waliongozwa na Afisa Mkuu (OCPD) wa Kibwezi Leonard Kimaiyo walifaulu kumsindikiza Bi Kiragu hadi katika afisi za shule hiyo hali iliyopelekea wanafunzi kuondoka madarasani wakipinga hatua hiyo. Wanafunzi hao waliounga mkono hatua ya madiwani hao huku wakiwashutumu polisi kwa kuwakamata wanasiasa hao.

"Tunataka Lucia arejeshwe!", wanafunzi hao waliimba wakirejelea mwalimu wao mkuu wa zamani Bi Lucia Roberts ambaye tayari amepewa uhamisho hadi Shule ya Upili ya Wavalana ya Nguviu.

Hata hivyo, baadhi ya walimu wao waliwakaripia vikali wakiwataka kudumisha utulivu na nidhamu.