http://www.swahilihub.com/image/view/-/2788134/medRes/1061356/-/r01isn/-/DNCOASTTOURISM2806B.jpg

 

Magavana Pwani wajadiliana na mabalozi kufufua utalii

Watalii watabaradi

Watalii wakitabaradi nje ya hoteli ya Serena Beach jijini Mombasa. Picha/KEVIN ODIT 

Na KALUME KAZUNGU

Imepakiwa - Monday, September 7  2015 at  10:30

Kwa Muhtasari

Magavana wote sita wa Ukanda wa Pwani wameanzisha mazungumzo na ofisi za ubalozi wa nchi mbalimbali za kigeni katika harakati za kuimarisha sekta ya utalii Pwani na Kenya kwa jumla.

 

MAGAVANA wote sita wa Ukanda wa Pwani wameanzisha mazungumzo na ofisi za ubalozi wa nchi mbalimbali za kigeni katika harakati za kuimarisha sekta ya utalii Pwani na Kenya kwa jumla.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Utalii na Wanyamapori katika baraza la Magavana na ambaye pia ni Gavana wa Lamu, Issa Timmamy, alisema mazungumzo hayo yanalenga hasa kuondoa marufuku iliyoko ya watalii kutoka nchi za nje kutozuru baadhi ya maeneo ya Pwani, ikiwemo Lamu na Malindi.

Dkt Timamy alitaja hatua ya kuendelea kuwekwa kwa marufuku ya watlii kutozuru baadhi ya maeneo ya Pwani kuwa kizingiti kikuu kinacholemaza juhudi za kuboreshwa kwa sekta ya utalii.

Alisema inasikitisha kwamba mataifa ya kigeni ikiwemo Uingereza na Marekani, bado yameshikilia marufuku ya watalii wake kutozuru Lamu na Malindi licha ya kwamba sehemu zote kwa sasa zinashuhudia amani na utulivu.

“Sifurahishwi na mataifa yanayozidi kushikilia marufuku ya watalii wao kutozuru Lamu na Malindi. Sisi magavana wote sita wa Pwani tayari tumeanzisha majadiliano na washikadau wakuu wa sekta ya utalii ili kuona kwamba marufuku hizo zinaondolewa mara moja. Mahali kama Lamu utalii bado ni ndoto kutokana na marufuku iliyopo. Nitafanya bidii kuhakikisha imeondolewa,” akasema Dkt Timamy.

Kwa upande wake, Naibu Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii wa Kaunti ya Lamu (LTA), Ghalib Ahmed Alwy, alikiri kwamba kutoondolewa kwa marufuku hiyo ni pigo kubwa kwa sekta ya utalii eneo hilo.

Bw Alwy alifichua kuwa tangu uvamizi wa kigaidi kutekelezwa kwenye maeneo ya Mpeketoni, Kibaoni, Witu na Hindi mnamo mwaka jana, utalii wa Lamu ulididimia kwa takriban asilimia 50.

Vile vile alisema kuendelezwa kwa marufuku ya watalii kutozuru Lamu kumeongeza zaidi dhana mbaya kwamba Lamu si salama, hivyo akayaomba mataifa husika kufikiria kuondoa marufuku hiyo mara moja ili kuiokoa sekta ya utalii aliyoitaja kuwa katika hatari ya kusambaratika.

"Lamu ni salama"

“Kisiwa cha Lamu ni salama. Mombasa, Nairobi na Kilifi zimewahi kushambuliwa na magaidi kwa gruneti lakini ndani ya mji wa Lamu bado. Sielewi ni kwa nini marufuku iendelezwe ndani ya kisiwa cha Lamu ilhali kuna amani. Tumeathirika pakubwa. Hoteli zimefungwa. Vijana wetu wamefutwa kazi na sekta ya utalii inazidi kudidimia kila kuchao. Vile mataifa husika yaliweza kuondoa marufuku ya watalii wake kuzuru maeneo ya Mombasa, Kilifi, Watamu na Kusini mwa Pwani, pia wafanye vivyo hivyo kisiwani Lamu,” akasema Bw Alwy.

Sekta ya utalii kaunti ya Lamu imekumbwa na misukosuko chungu nzima hasa tangu uvamizi wa kigaidi kutekelezwa na majangili wa Al-Shabaab eneo hilo, na kupelekea vifo vya watu zaidi 90 na mali ya mamilioni ya fedha kuteketezwa kati ya Juni na Julai 2014.

Ikiwa majadiliano ya washikadau wa utalii na magavana yatafaulu kuondoa marufuku iliyoko ya watalii, basi huenda mwamko mpya wa utalii ukashuhudiwa Pwani na Kenya kwa jumla.