http://www.swahilihub.com/image/view/-/4260676/medRes/1856767/-/f8vh5vz/-/ww.jpg

 

Mageuzi shuleni yageuka balaa

Urbanus Wambua

DIWANI Mteule wa Chama cha Wiper Kaunti ya Makueni, Urbanus Wambua (asiye na shati), apambana na polisi katika Shule ya Upili ya Wasichana ya St Joseph’s, eneo la Kibwezi, fujo zilipozuka kati ya madiwani na maafisa wa elimu wa kaunti hiyo kuhusu mwalimu mkuu mpya Januari 11, 2018. Picha/ PIUS MAUNDU 

Na WAANDISHI WETU

Imepakiwa - Thursday, January 11  2018 at  21:46

Kwa Muhtasari

MAGEUZI yaliyofanywa na Wizara ya Elimu ya kuhamisha walimu wakuu 555 kote nchini yamezua mgogoro mkubwa nchini, ambapo wanasiasa, wazazi, wakazi na wanafunzi wanaendelea kuwafurusha walimu hao.

 

Tukio la punde zaidi ni la Alhamisi ambapo kulizuka makabiliano makali katika shule moja Kaunti ya Makueni, baina ya madiwani sita na polisi.

Madiwani hao, ambao baadaye walikamatwa na polisi, walivamia Shule ya Upili ya Wasichana ya St Joseph’s Kibwezi, na kupinga vikali kuwasili kwa mwalimu mkuu mpya wa shule, Bi Rose Kiragu.

Wanafunzi wa shule hiyo pia walionyesha kutoridhishwa na kuondolewa kwa mwalimu mkuu waliyemzoea kwa kususia masomo.

Hiyo Alhamisi, polisi katika kaunti ya Bungoma walikuwa wakiwasaka madiwani wanne ambao walimuondoa kwa lazima mwalimu mkuu mpya wa Shule ya Msingi ya Wavulana ya Friends’ School Kamusinga.

Madiwani hao, Elvis Abuka, Stephen Wamalwa (Soysambu/Mitua), Aggrey Mulongo (Kibingei) na Diwani Mteule, Luke Opwora, walivamia shule hiyo Jumatano na kumuondoa Bw Alex Kariuki Maina.

Gavana Wycliffe Wangamati aliunga mkono hatua hiyo akisema alisema mwalimu huyo alishindwa kuimarisha viwango vya elimu katika shule aliyotoka.

“Hatutakubali mwalimu mkuu kutoka shule iliyo na alama za wastani 5.9 kusimamia shule iliyo na alama za wastani 9.2. Walimu wakuu hao wahamishiwe shule wanazoweza kuongoza,” akasema Bw Wangamati.

Mwalimu huyo na walinzi wa shule hiyo waliandikisha taarifa katika Kituo cha Polisi cha Kimilili.

Hiyo hiyo Alhamisi, wazazi waliojawa na hasira katika Kaunti ya Migori walimtimua mwalimu mkuu wa Shule ya Upili ya Nyagere, eneo la Nyatike. Walimfungia nje ya shule wakisema kwa miaka 10 iliyopita shule hiyo haijawa na matokeo mazuri.

Shule zingine ambazo zimekumbwa na hali sawa katika kaunti hiyo ni Kanga Onditi, Obolo, Okuodo, na Nyemataburo.

Mgogoro huo ulianzia Kaunti ya Pokot Magharibi ambako Bw Julius Mambili kutoka Shule ya Upili ya Kabarnet alipelekwa shule ya Kapenguria iliyokuwa ikisimamiwa na Bw James Omayo.

Mwenyekiti wa Chama cha Walimu (Kuppet) tawi la Trans Nzoia, Eliud Wafula, alidai kuwa Bw Mambili alishindwa kuingia shuleni humo baada ya kupata lango limefungwa kwa minyororo.

Mnamo Januari 8, wazazi wa Shule ya Upili ya St Joseph’s Githunguri, Kiambu, nao waliandamana kupinga kuhamishwa kwa Mwalimu Mkuu, Moses Muiruri, hadi Shule ya Upili ya Kaheti Boys, Mukurweini, Kaunti ya Nyeri, wakisema mwalimu huyo amehudumu katika shule hiyo kwa miaka miwili pekee na kumhamisha ni kuhujumu masomo katika shule hiyo.

Kufuatia kisa hicho, shule hiyo ilifungwa kwa muda usiojulikana.

Wizara ya Elimu imewahamisha walimu wakuu waliohudumu katika shule moja kwa zaidi ya miaka tisa, huku shule za kitaifa 31 zikiathirika katika mpango huo.


Ripoti za Faustine Ngila, Gerald Bwisa, Titus Oteba, Oscar Kakai, Pius Maundu, Wanderi Kamau na
Elisha Otieno