Wenye matatu wataka maisha ya polisi wa trafiki yachunguzwe

Na CAROLYNE AGOSA

Imepakiwa - Thursday, December 7  2017 at  18:43

Kwa Muhtasari

WAMILIKI wa matatu nchini wanataka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuanzisha uchunguzi wa maisha ya polisi wa trafiki kama njia moja ya kukabiliana na ufisadi uliokithiri katika sekta hiyo ya uchukuzi wa umma.

 

Vile vile, wanataka ofisi hiyo kuwasilisha marekebisho ya sheria ili kuruhusu picha za polisi wakipokea hongo kutumika kama ushahidi kortini dhidi ya maafisa wafisadi.

Wakizungumza Jumatano mjini Nairobi kupitia Chama cha Wamiliki wa Matatu (MOA), wamiliki hao walisema uchunguzi huo wa maisha ya polisi utasaidia kuwanasa maafisa ambao wamekuwa wakijinufaisha na hongo wanazochukua kila siku kutoka kwa matatu.

“Polisi wengi wa trafiki wanaishi maisha ya juu isivyoambatana na kiwango cha mishahara wanayopokea. Unapata afisa wa trafiki anamiliki mali ya mamilioni ya pesa ilhali mshahara wake hauwezi kamwe kumudu hali hiyo ya maisha,” alisema mwenyekiti wa MOA, Simon Kimutai.

“Mambo yakiendelea hivi biashara ya matatu itasambaratika na hatutaweza kutoa huduma kwa wananchi kwani hatutakuwa na pesa za kukarabati magari, kulipa mikopo na ada zingine.”

Wamiliki hao wa matatu walikuwa wakizungumza katika warsha ya siku moja ya iliyoandaliwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).

Waliomba mahakama kupunguza faini zinazotolewa dhidi ya wahudumu wa matatu hususan kwa makosa madogo, na pia kuondoa dhamana za pesa kama njia ya kuzuia maafisa wa trafiki kuwashika mateka wahudumu hao.

Kwa upande mwingine, walilalamikia kucheleweshwa kwa kesi za maafisa wa trafiki ambazo mwishowe hutupwa nje ama maafisa hao kupewa adhabu finyu.

Hatua hiyo huwafanya wadokezi kukata tamaa ya kupiga ripoti zozote za ufisadi kwa kuhofia kuhangaishwa na maafisa husika.

Afisa Mtendaji wa EACC Dkt Halakhe Waqo aliahidi kushughulikia ripoti zote zitakazowasilishwa kwa tume.

Pia “tuko mbioni kufanya marekebisho ya sheria za kupambana na ufisadi kuhakikisha mfumo wa sheria ni thabiti kabisa kukabiliana na kuzuia ufisadi katika sekta ya matatu,” akasema katika taarifa iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Uchunguzi EACC, Bw Abdi Muhamud.

Idara ya polisi imejipata pabaya kwa kuongoza orodha ya ufisadi kwa miaka mingi huku maafisa hao wakishutumiwa kwa kujali vyao vya tumboni badala ya kudumisha usalama barabarani.