http://www.swahilihub.com/image/view/-/2485492/medRes/850011/-/bdkteoz/-/DNLAMULAND2409ce.jpg

 

Wanyakuzi wa ardhi Mama Ngina Drive wapewa siku 90 wawe wameondoka

Mohammed Swazuri

Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) Mohammad Swazuri Picha/MAKTABA 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Thursday, January 10  2019 at  12:34

Kwa Muhtasari

Tume ya kitaifa ya ardhi nchini, NLC, Alhamisi imezuru bustani ya Mama Ngina iliyopo kaunti ya Mombasa.

 

MOMBASA, Kenya

TUME ya kitaifa ya ardhi nchini, NLC, Alhamisi imezuru bustani ya Mama Ngina iliyopo kaunti ya Mombasa.

Mwenyekiti wake Mohamed Swazuri ameongoza makamishna wenza kutathmini ardhi ya bustani hiyo iliyonyakuliwa.

Bustani ya Mama Ngina ina ukubwa wa ekari 26, na kulingana na Swazuri baada ya kupekua stakabadhi ni kwamba ekari 20 ndizo zimenyakuliwa na wawekezaji wa kibinafsi.

Akiongea na waandishi wa habari, mwenyekiti huyo amesema unyakuzi huo ulitekelezwa kati ya mwaka wa 1985-2012.

"Kwa jumla ya ekari 26, 20 zimenyakuliwa na wawekezaji wa kibinafsi. Shughuli hii haramu na inayokiuka sheria ilifanywa kati ya 1985-2012. Ekari sita pekee ndizo zimesalia," amesema Swazuri.

Swazuri na makamishna wenza wa tume hiyo waliandamana na baadhi ya maafisa kutoka wizara ya ardhi nchini na waziri wa ardhi kaunti ya Mombasa.

Ziara ya NLC katika bustani hiyo inajiri kufuatia agizo la Rais Uhuru Kenyatta la mnamo Jumatatu, akiitaka tume hiyo na wizara ya ardhi kushirikiana kuhakikisha ardhi iliyonyakuliwa imerejeshwa mikononi mwa umma.

Akizindua ukarabati upya wa Mama Ngina utakaogharimu kima cha Sh460 milioni, Rais alitoa makataa ya chini ya miezi sita ardhi iliyonyakuliwa irejeshwe. Ujenzi wake utajumuisha mikahawa na majumba ya kisasa ya kibiashara, yanayopaniwa kupiga jeki utalii Pwani na Bw Kenyatta anatarajiwa kuzindua ung'oaji nanga wa biashara Juni 2019.

Hatimiliki

Swazuri ameambia waandishi wa habari kuwa hatimiliki 13 zilitolewa kwa ekari 20 zilizonyakuliwa.

Wanyakuzi wamepewa makataa ya siku 90 kuondoka katika ardhi hiyo, pamoja na kurejesha hatimiliki walizokabidhiwa na vyeti vyovyote vinavyoonesha walivyopata umiliki.

"Ardhi ya Mama Ngina ni ya umma, haifai kunyakuliwa. Tunatoa notisi kwa wanyakuzi kwa mujibu wa kifungu 155 cha sheria za mashamba, na marekebisho yake 152 (a-c), warudishe hatimiliki na stakabadhi walizopewa. Tumewapa siku 90 wawe wameondoka," ameeleza Swazuri.

Aliongeza kusema kuwa Jumanne wiki ijayo, NLC itachapisha makataa haya kwenye magazeti.

Wakati wa uzinduzi wa ukarabati wa Mama Ngina, gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho alisema serikali yake inasubiri tume ya ardhi nchini na wizara husika iipe mwelekeo ili ubomoaji wa majengo ya wanyakuzi uanze.

Visa vya mashamba Pwani kunyakuliwa si vigeni, mwaka uliopita ardhi ya eneo taka la Kibarani ilirejeshwa kufuatia agizo la Rais na shinikizo la serikali ya kaunti ya Mombasa.