http://www.swahilihub.com/image/view/-/4112624/medRes/1763246/-/15n6io2z/-/maraf.jpg

 

Maraga afurahia kazi ya wanahabari nchini Kenya

David Maraga

Jaji Mkuu wa Kenya, David Maraga. Picha/MAKTABA 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Wednesday, June 13  2018 at  16:18

Kwa Muhtasari

Jaji Mkuu nchini Kenya amesema kuna haja ya kutambua juhudi za vyombo vya habari kutokana na kazi ambayo vinafanya.

 

NAIROBI, Kenya

JAJI Mkuu (CJ) David Maraga amesema kuna haja ya kutambua juhudi za vyombo vya habari kutokana na kazi ambayo vinafanya.

Aidha, jaji huyo amepongeza waandishi wa habari nchini akisema hujitolea mhanga kuhakikisha taifa limeelimika, na kupokea matukio maalum yanapojiri.

Akihutubu kwenye mkutano wa muungano wa wahariri nchini (Editors Guild) mnamo Jumanne, Bw Maraga alisema vyombo vya habari na waandishi wake wana kila sababu ya kupigiwa upatu ikizingatiwa kuwa wengine hujipata katika hali tata wakitekeleza majukumu yao.

"Vyombo vya habari na waandishi wake humu nchini kwa jumla wanafanya kazi bora. Mfahamu kuwa taifa linawategemea kupashwa habari," akasema, kwenye mkutano huo ulioandaliwa jijini Nairobi.

Jaji huyo alieleza haja ya haki za waandishi wa habari kuheshimiwa, akiahidi kuwa idara yake itafanya kazi kwa karibu na wanahabari.

"Idara ya mahakama inatambua majukumu ya wanahabari Kenya, hivyo basi itasimama kidete nao," akasema.

Nchini kuna zaidi ya vyombo 50 vya habari, ikijumuisha redio, na runinga. Hata hivyo, mitandao ya kijamii kama Twitter, Facebook na Instagram inaonekana kuwa kipau mbele katika upashaji wa habari ibuka.

Baadhi ya waandishi wa habari nchini na kimataifa, wamejipata kudhulumiwa na maafisa wa polisi, wanasiasa na hata umma wakitekeleza majukumu yao. Vyombo vya habari vimesaidia kulainisha serikali tawala, hasa katika kufichua visa vya ufisadi miongoni mwa watumishi wa umma.

Kadhalika, vimechangia pakubwa kufichua maovu yanayofanyika katika jamii na hata kutetea haki za raia, kama kunyanywa kwa watoto na wanawake.

Mbali na muungano wa wahariri, baraza la vyombo vya habari (MCK), na muungano wa waandishi wa habari (KNUJ) ndio taasisi za kujitegemea zinazotetea haki za wanahabari Kenya.