http://www.swahilihub.com/image/view/-/4801410/medRes/2137640/-/5q4ry5z/-/maranga.jpg

 

Maraga awapa majaji rungu kuamua kesi za mashamba

Jaji Mkuu (CJ) David Maraga  

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Thursday, October 11  2018 at  15:09

Kwa Muhtasari

Mahakama ina kesi milioni 5 zinazohusu mizozo ya mashamba

 

Nyeri. Upungufu wa majaji nchini ndio kiini cha msongamano wa kesi mahakamani, amesema Jaji Mkuu (CJ) David Maraga.

Kwenye ziara yake kaunti ya Nyeri mnamo Alhamisi, Jaji Maraga alisema mrundikano wa kesi zilizoko mahakamani utapunguzwa kwa kuajiri mahakimu na majaji.

Alisema malalamishi ya kesi za mashamba ndiyo yanaongoza kwa orodha ya kesi zilizoko mahakamani. Aidha, Maraga alitangaza kwamba mahakimu sasa wanaruhusiwa kusikiliza na kutoa uamuzi wa kesi hizo.

"Kesi za mashamba ni nyingi sana katika korti zetu, na tunajaribu kama idara ya mahakama kuzipunguza. Tumewapa mamlaka mahakimu kuzisikiliza na kuziamua," alisema Maraga.

Aliongeza: "Tuna zaidi ya kesi milioni 5 zinazohusu mizozo ya mashamba. Kinachohitajika ni kuwa na mahakimu na majaji wa kutosha katika korti zetu." Maraga alikuwa ameandamana na msajili mkuu wa mahakama Anne Amadi.

Jaji huyu pia alitaja ukosefu wa ufadhili wa kutosha kama kizingiti kikuu cha huduma bora katika idara ya mahakama. Baada ya makadirio ya bajeti Mwaka wa Fedha 2018/2019 kusomewa, Jaji Maraga alipuliza kipenga akidai kuwa mgao ambao idara yake ilipokea ni haba mno ikilinganishwa na bajeti yake.

Hata hivyo, serikali iliahidi kwamba itatathmini suala la kuiongezea fedha ili kuiwezesha kuendesha majukumu yake kikamilifu. Idara ya mahakama inategemewa pakubwa katika vita dhidi ya ufisadi nchini.