Mataifa kukutana Geneva kujadili magonjwa ya tropiki

Na  BERNARDINE MUTANU

Imepakiwa - Thursday, April 20  2017 at  18:14

Kwa Mukhtasari

Ulimwengu unakutana Geneva, Switzerland, kujadili magonjwa ambayo yamepuuzwa katika maeneo ya joto au tropiki (NTD).

 

Kenya ni miongoni mwa mataifa ya tropiki na ambako magonjwa hayo yalikuwa yamepuuzwa. Magonjwa hayo ni kama ugonjwa wa malale na homa ya dengue.

Viongozi hao walitangaza tena kujitolea kwao kumaliza magonjwa hayo na kuelezea kuwa hatua kubwa imepigwa tangu kampeni ya kuyamaliza ilipoanzishwa mwaka wa 2012.

Serikali na wafadhili walitoa ahadi ya Dola 812 milioni wakati wa mkutano huo wa siku tano unaoendelea Geneva juma hili.

Mkutano huo ulifanyika kuambatana na uzinduzi wa Ripoti ya Nne ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO)  kuhusiana na magonjwa ya NTD.

Uingereza ilitoa ahadi ya kutoa ufadhili maradufu wa kukabiliana na magonjwa hayo. Mkutano huo umefanyika miaka mitano tangu kuzinduliwa kwa mkataba wa London kumaliza magonjwa ya NTD mwaka wa 2012.

Kati ya watu maarufu waliohudhuria ni mfadhili wa kampeni dhidi ya magonjwa tofauti na mwekezaji maarufu  Bill Gates chini ya wakfu wa Bill & Melinda Gates Foundation.