http://www.swahilihub.com/image/view/-/4144500/medRes/1784007/-/80yhhdz/-/gafa.jpg

 

Mataifa ya Magharibi ni wanafiki - Raila

Raila Odinga

Kiongozi wa Nasa, Raila Odinga. Picha/SALATON NJAU 

Na WANDERI KAMAU

Imepakiwa - Thursday, December 7  2017 at  18:57

Kwa Muhtasari

KINARA wa NASA, Raila Odinga, ameshambulia vikali mataifa ya Magharibi, akiyataja kuwa wanafiki kwa kunyamaza polisi walipokuwa wakiwaua wafuasi wake kwa risasi.

 

Bw Odinga alisema kuwa ni kinaya kwa nchi hizo kunyamaza mauji hayo yakiendelea licha ya kushikilia kuwa “marafiki wa Kenya.”

Akihutubu Alhamisi katika Mochari ya City, jijini Nairobi, familia za waathiriwa zilipochukua miili 16 iliyobaki, Bw Odinga alilalamika kwamba nchi hizo hazina sababu yoyote ya kuwataka Wakenya wazingatie sheria akisema zimeonyesha mapendeleo ya wazi kwa serikali ya Jubilee.

“Ni kinaya kwa nchi hizo na mabalozi wake kutuambia tuzingatie sheria ilhali mamia ya watu wameuawa na polisi huku zikitazama bila kutoa kauli yoyote. Huo ni unafiki wa wazi,” akasema.

Alidai kwamba watu 215 wameuawa na polisi tangu Agosti 8 na kusikitika kwamba hakuna afisa yeyote wa serikali aliyejitokeza kulaani mauaji hayo au hata kufariji familia za waathiriwa.

Idadi hiyo inatofautiana na ya mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu ambayo yamesema kuwa watu 37 waliuawa katika kipindi hicho cha uchaguzi.

Bw Odinga aliitaka serikali ijitokeze wazi kuwaomba Wakenya msamaha kwa vifo hivyo anavyodai vilitekelezwa na polisi kwa maagizo ya wakubwa wao.

Alisema kuwa ni lazima waliohusika wawajibike kwa sababu haiwezi kuwa jambo la kawaida kwa mauaji kutekekezwa bila hatua kuchukuliwa kwa wanaohusika.

Kiongozi huyo wa Upinzani alishikilia kuwa muungano huo haumtambui Rais Uhuru Kenyatta akitaja uchaguzi wa urais wa Oktoba 26 kuwa “shughuli ya Jubilee.”

“Msimamo wetu ni kwamba hakukuwa na uchaguzi wowote Oktoba 26. Kenya kwa sasa haina rais halali kikatiba,” akasema.

Bw Odinga ameshikilia kuwa ataapishwa rasmi Desemba 12 kuwa “Rais wa Wananchi”.

Wiki iliyopita, miili 10 ya watu waliouawa katika kipindi cha uchaguzi ilikabidhiwa familia zao na kusafirishwa maeneo tofauti nchini kwa mazishi.

Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Nairobi, Bi Esther Passaris, alishikilia kuwa wafuasi wao hawakufanya makosa yoyote walipojitokeza kuandamana.

Miongoni mwa miili iliyotolewa ni ya mtoto Geoffrey Mutinda, mwenye umri wa miaka saba, anayedaiwa kuuawa na polisi katika Mtaa wa Pipeline, Nairobi, mwezi uliopita, kwenye makabiliano na wafuasi wa NASA.

Kila familia ilipewa Sh50,000 ili kugharamia mazishi na usafirishaji wa miili.

Baadhi ya viongozi walioandamana na Bw Odinga ni Seneta James Orengo (Siaya), wabunge Millie Odhiambo (Mbita), Otiende Amollo (Rarienda), Simba Arati (Dagoretti Kaskazini) na aliyekuwa Seneta wa Machakos, Johnstone Muthama miongoni mwa wanasiasa wengine wa muungano wa NASA.