Matiang'i asema wahalifu wanajifanya waandamanaji wa kupinga matokeo ya kura za urais

Dkt Fred Matiang'i

Kaimu Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang'i ahutubia wanahabari Agosti 12, 2017 katika jumba la Harambee. Pamoja naye ni viongozi wengine serikalini. Picha/ROBERT NGUGI 

Na MWANGI MUIRURI na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Saturday, August 12  2017 at  13:02

Kwa Mukhtasari

Kaimu Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i ametoa onyo kuwa maafisa wa polisi hawatawapa nafasi majambazi kuteka nyara harakati za hisia baada ya uchaguzi kutekeleza ukora wao katika jamii.

 

KAIMU Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i ametoa onyo kuwa maafisa wa polisi hawatawapa nafasi majambazi kuteka nyara harakati za hisia baada ya uchaguzi kutekeleza ukora wao katika jamii.

Matiang’i amesema kuwa njama ya majambazi hao ni kujifanya kama waliokerwa na matokeo ya uchaguzi huo mkuu kama yalivyotolewa rasmi na tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) na kama njia ya kulalamika, wanatokea mitaani kupora biashara za wenyewe.

“Serikali haitakubali magenge hayo kutekeleza njama hiyo yao na kwa sasa tunajua visa vinavyoshuhudiwa katika maeneo kadhaa hapa nchini na ambavyo wengine wanavitaja kama ghasia za uchaguzi ni njama ya mitandao hiyo ya ujambazi,” amesema Matiang'i akihutubu Jumamosi katika jumba la Harambee jijini Nairobi.

Matiang’i ameonya baadhi ya walio na akaunti katika mitandao ya kijamii kuwa wataandwamwa ikiwa itathibitika kuwa wanaeneza uvumi usio
na msingi kuhusu hali ya usalama hapa nchini.

"Hadi kufikia sasa tumefahamishwa na Inspekta Mkuu wa Polisi, Joseph Boinnet kuwa kuna kadhaa ambao wamenaswa na tutaendelea kutekeleza msako huo ili kuzua hali ya uthabiti kuhusu hali ya usalama,” amesema.

Ameonya pia wanasiasa wawe wa kuwajibikia usalama “hasa wale ambao walipoteza kwenye uchaguzi huo wa Agosti 8, 2017”.

Akasema: “Kwa upande wetu wa serikali, mlimsikia Naibu wa Rais William Ruto alipopiga kura yake Agosti 8 akisema kuwa ni lazima tujumuike pamoja kama Wakenya bila kuzingatia matokeo ya kura hiyo. Alikuwa muwazi kabisa kuwa cha maana ni kuhakikishia taifa hili umoja wake na amani kwa wote.”

Alisema hata Rais Uhuru Kenyatta akitoa hotuba yake baada ya kutangazwa mshindi na IEBC Ijumaa usiku alisema kuwa kuna umuhimu wa wadau wote katika ushindani wa Agosti 8 waje pamoja na wajadiliane kuhusu umoja wa taifa hili na amani yake.
Matiang'i anadai yumkini matukio machache ya vijana kuonekana barabarani wakizua rabsha "yamepangwa kisiasa".

Alisema kuna haja kwa vyombo vya habari kuwajibikia usahihi wa habari ili kuepukana na tishio la kusambaza habari za uongo na ambazo hazijathibitishwa hivyo basi kusambaza hali ya taharuki nchini.

Alilalamika kuwa kuna baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vinatumia picha za ghasia za 2007 na hata picha za matukio ya nje ya nchi kujaribu kueneza uvumi kuwa ni hali ilivyo kwa sasa.

Akisema kuwa maandamano ya amani hayatazimwa na polisi bora tu yaandaliwe kwa msingi unaokubalika kisheria, alisema vinginevyo matukio mengine yataorodheshwa kama ya kijambazi.

Kwa mantiki hiyo Kaimu Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang'i amesema kuwa usalama ni shwari kote nchini.

Amesema hali ya mshikemshike iliyoanza kushuhudiwa tangu Alhamisi mitaani Kibera na Mathare Kaunti ya Nairobi na baadhi ya Maeneo Kaunti ya Kisumu, inasababishwa na waandamanaji ambao ni 'wezi na waporaji' mali ya umma na kwamba maandamano yao si ya halali wala ya amani kwa kuwa wamekiuka kanuni za sheria.

"Watu wanaovunja maduka na nyumba za watu ili kuiba mali, kupiga wengine, na kuchoma magari si waandamanaji wa amani," amesema Dkt Matiang'i.

Hii ndio imekuwa hotuba yake ya kwanza baada ya Rais Uhuru Kenyatta wa Jubilee na Naibu wake William  Ruto kutangazwa kuwa washindi kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika kote nchini mnamo Jumanne Agosti 8, 2017.

Maandamano hayo aidha yalizidi mnamo Ijumaa usiku baada ya Rais Kenyatta kutangazwa kuwa mshindi na mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC Bw Wafula Chebukati katika Ukumbi wa Bomas of Kenya Nairobi, kwenye uchaguzi huo ambapo ataongoza taifa hili kwa kipindi cha miaka mingine mitano ijayo baada ya kuzoa kura 8,203,290 ikiwakilisha asilimia 54.24 na kinara wa muungano wa National Super Alliance (Nasa) Raila Odinga akipata kura 6,762,224 ikiwa ni asilimia 44.74 kwa jumla ya kura 15,073,662 zilizopigwa na kuwakilisha asilimia 78.91 ya wapiga kura 19,687,563 waliosajiliwa na tume ya IEBC.

Haki ya kuandamana

Dkt Matiang'i amedokeza kuwa maandamano yaliyo halali na ya amani huwa na ulinzi wa polisi kwa mujibu wa katiba.

"Katiba inaruhusu kila mwananchi afanye maandamano kwa amani, ambayo huwa na ulinzi," ameeleza.

Amekanusha kuwa maafisa wa polisi wanaoshika doria katika maeneo hayo wanatumia nguvu kupita kiasi kutuliza ghasia zilizozuka.

"Maafisa wetu wamepokea mafunzo ya kulinda wananchi ila si kuwadhuru. Kumekuwa na uvumi kuwa polisi wanatumia nguvu kutawanya wanaoandamana kinyume cha sheria, huo ni uvumi mtupu," akaeleza.

Akaongeza: "Hakuna afisa wa polisi ambaye amepiga risasi wanaoandamana kwa amani."

Amepinga vikali kuwa kuna baadhi ya wananchi waliouawa kwenye ghasia hizo akidokeza kwamba Inspekta Jenerali Mkuu wa Polisi Joseph Boinnet angekuwa ametoa taarifa.

"Tulikuwa na mkutano wa usalama na Inspekta Boinnet leo asubuhi (Jumamosi), hakuna jambo kama hilo la mauaji limetokea. Sina habari ya yeyote aliyeuawa kwa kupigwa risasi nchi hii. Nina furaha kwa sababu mnatumia majina 'uvumi unasema' na hatuegemei uvumi ila ukweli," akasema akijibu maswali tata ya wanahabari kwamba kuna baadhi ya watu waliouawa kwa kupigwa na maafisa wa polisi, habari ambazo hazijathibitishwa na yeyote.

"Tuna uhakika na tunayosema, nchi yetu ni salama mbali na visa vichache vya Kibera, Mathare katika Kaunti ya Nairobi na baadhi ya maeneo Kisumu. Wananchi wenzangu, tuishi kama ndugu na dada," akaongeza akisisitiza kauli ya Rais Kenyatta ya mnamo Ijumaa baada ya kutangazwa mshindi kwamba 'amani idumishwe nchini'.

Waziri Matiang'i ameongeza kuwa wanaoeneza jumbe za chuki, ukabila na ghasia kwenye mitandao ya kijamii watachukuliwa hatua kali kisheria. "Tunafuatilia mitandao ya kijamii na kufikia sasa kuna waliotiwa nguvuni kwa kueneza jumbe za chuki, ukabila na ghasia," amefichua.

Amepongeza vyombo vya habari vinavyofanya kazi bora kwa kueneza habari za amani na zinazofaa, ingawa ameonya vichache vinavyoonyesha video za kitambo za ghasia.

"Kuna vyombo vya habari vinavyoonyesha video za kitambo za maandamano na mashambulizi, tunavionya tutavifikia na kuvichukulia hatua kisheria," akasema.

Haya yanajiri wakati ambapo ripota wa runinga moja nchini Kenya akiwa ametiwa nguvuni Jumamosi asubuhi kwa kuvalia magwanda ya polisi wakati akiripoti maandamano yaliyofanyika Kibera, Nairobi, maafisa wa polisi aidha walilazimika kutumia vitoa machozi ili kutuliza ghasia.

Hata hivyo, Dkt Matiang'i amepongeza maafisa wa usalama kwa kuimarisha usalama kote nchini tangu uchaguzi ulipofanyika mnamo Jumanne.

"Ninapongeza wananchi kwa kushirikiana na maafisa wa polisi ili kuimarisha usalama nchini. Naomba kila mtu arejee kazini, uchaguzi umeisha," akasema.

Zaidi ya maafisa 180,000 wa usalama ndio walitumwa katika maeneo mbali mbali kote nchini ili kushika doria kabla, wakati na baada ya uchaguzi.