http://www.swahilihub.com/image/view/-/4115758/medRes/1233939/-/9imxm7/-/DNDIGITAL1512j.jpg

 

Matiang'i asisitiza ni sharti nidhamu irejeshwe barabarani

Fred Matiang'i

Dkt Fred Matiang'i akihutubu awali. Picha/GERALD ANDERSON 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Friday, November 9  2018 at  18:07

Kwa Muhtasari

Ajali zimekuwa zikishuhudiwa nchini Kenya mara kwa mara katika kile kinatajwa ni kulegezwa kwa sheria za barabarani.

 

NAIROBI, Kenya

SHERIA za trafiki zilizoanzishwa na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi John Michuki lazima ziteketelezwe bila kusita, amesema Dkt Fred Matiang'i.

Waziri huyu wa Usalama wa Ndani mnamo Ijumaa amesema sheria hizi zinapania kurejesha nidhamu barabarani. Amesema kiwango cha nidhamu miongoni mwa wahudumu wa matatu na bodaboda kimemomonyoka, kiasi kwamba kisipodhibitiwa  huenda taifa likajipata pabaya.

Akihutubu kwenye mkutano na vigogo wa usalama kutoka kaunti zote 47, uliofanyika katika Taasisi ya Mafunzo ya Kiserikali, KSG, jijini Nairobi, Dkt Matiang'i amesema ongezeko la visa vya ajali nchini linatokana na utepetevu wa wahudumu hawa.

"Tunataka kurejesha nidhamu katika sekta ya usafiri na uchukuzi. Tusipofanya hivyo, hatutaweza kuidhibiti tena kutokana na mkondo inaoelekea," alionya waziri huyu.

Akionekana kughadhabishwa na mienendo ya wendeshaji bodaboda, Bw Matiang'i amesema operesheni ya kushinikiza sheria za Michuki kutekelezwa inayotarajiwa kuanza rasmi Jumatatu ijayo haitagusa wahudumu wa matatu pekee ila mpaka wa bodaboda.

Alisema msako dhidi ya magari yanayokiuka sheria za trafiki na za halmashauri ya uchukuzi na usalama wa kitaifa (NTSA) unaoendelea jijini Nairobi ni kionjo tu, na kwamba operesheni ya Jumatatu 'itasafisha' sekta ya usafiri na uchukuzi.

"Lazima tubadilishe mambo, hatutaendelea na yalivyo kwa sasa. Msako tulioanza ni kionjo tu," amesema.

Hata hivyo, muungano wa wamiliki wa matatu nchini, MOA, unakosoa oparesheni hii inavyoendeshwa.

Sheria za Michuki zilizinduliwa mwaka wa 2003 na zinahitaji matatu iwe na kidhibiti mwendo, mikanda, mstari wa manjano ambapo katika rangi hiyo pawepo maandishi ya ruti inakohudumu matatu, madereva na utingo wawe na sare maalum, miongoni mwa zingine.

Kibali cha kuhudumu

Pia, zinajumuisha vigezo vya halmashauri ya uchukuzi na usalama wa kitaifa (NTSA) ambapo kila gari la umma linatakiwa kuwa na kibali cha kuhudumu pamoja na dereva wake na vinginevyo.

Oktoba 2018, taifa lilipoteza watu si chini ya 58; ambapo ripoti zaidi zilileza ilifikia watu 62 katika ajali ya barabara eneo la Fort Ternan, Kericho iliyohusisha basi la Home Boyz.

Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma, DPP, Noordin Haji mapema Ijumaa ameagiza Inspekta Mkuu wa Polisi (IG) Joseph Boinnet kufanya uchunguzi wa kampuni iliyounda basi hilo pamoja na iliyoipa bima.

Dkt Matiang'i ameeleza kufurahishwa kwake na hatua ya DPP, akieleza haja ya kampuni za bima kupigwa msasa.

"Ninaunga mkono hatua ya DPP, kampuni za kuunda magari na kusajili bima siku zao zimehasibiwa. Ajali nyingi zimefanyika nchini na hawafidii waathiriwa, afadhali tuachanie kortini," amesisitiza Matiang'i.

Waziri wa Uchukuzi James Macharia amesema ufufuzi wa sheria za Michuki utaleta mabadiliko makuu katika sekta ya usafiri na uchukuzi. Alisema sheria za trafiki sharti zitiliwe maanani kwa vyovyote vile kwa ajili ya usalama barabarani.

"Tunayofanya yataleta mageuzi makuu katika barabara zetu ili maisha yetu yawe salama tunaposafiri," alieleza.

Matiang'i alikuwa ameandamana na katibu katika wizara yake, Dkt Karanja Kibicho. Mbali na vigogo wa usalama nchini, mkutano huo pia ulihudhuriwa na waratibu wa maeneo na kaunti. 

Marehemu Michuki anakumbukwa kwa hili.