Julius Mawathe aidhinishwa na Wiper kutetea kiti chake Embakasi Kusini

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Wednesday, January 30  2019 at  10:20

Kwa Muhtasari

Aliyekuwa mbunge wa Embakasi Kusini Julius Mawathe Jumanne amekabidhidiwa na Wiper Party tiketi ya kuwania kutetea kuhifadhi kiti chake.

 

NAIROBI, Kenya

ALIYEKUWA mbunge wa Embakasi Kusini Julius Mawathe Jumanne amekabidhidiwa na Wiper Party tiketi ya kuwania kutetea kuhifadhi kiti chake.

Hii ni baada ya mahakama ya juu zaidi nchini Desemba 12, 2018, kufutulia mbali rufaa aliyowasilisha kupinga uamuzi wa mahakama ya rufaa. Aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Irshad Sumra Mohammed, alifanikiwa kupinga ushindi wa Mawathe wa Agosti 7, 2017, katika mahakama kuu na ile ya rufaa.

Kwenye uamuzi wake, mahakama ya juu ilibatilisha ushindi wa Bw Mawathe ikieleza matokeo yaliyotangazwa baada ya Agosti 8 hayakuwa na ushahidi wa kutosha kudhihirisha kuwa aliibuka mshindi. 

Mahakama hiyo ilisema tume huru ya uchaguzi na uratibu wa mipaka (IEBC) haikuwasilisha fomu halisi ya 35A, hivyo basi kutilia shaka ushindi wa Mawathe.

Wiper imesema mbunge huyu atawania kuhifadhi kiti chake kupitia chama hiyo. "Uchaguzi uliopita Julius Mawathe alipita kwa zaidi ya kura 30,000, mara hii ataibuka mshindi kwa zaidi ya kura 50,000. Ninasihi wapiga kura wajitokeze kwa wingi," akasema kiongozi wa Wiper Kalonzo baada ya kukabidhi mgombea huyo cheti, katika afisi za chama hicho jijini Nairobi.

Kura

Katika uchaguzi huo, Mawathe aliibuka mshindi kwa kuzoa kura 33,880 dhidi ya mpinzani wake wa karibu Sumra (ODM) aliyepata 33,708.

IEBC imepanga uchaguzi mdogo wa eneobunge hilo kufanyika Aprili 5 mwaka huu. Chama tawala cha Jubilee kimetangaza kuwa hakiwasilisha mgombea wake, hivyo basi hakitashiriki katika zoezi hilo. Hakijatangaza kinayeunga mkono.