http://www.swahilihub.com/image/view/-/1412060/medRes/363143/-/k2gow4/-/DnRaila2005t.jpg

 

Mgawanyiko wa mawakili wa NASA ulivyomchelewesha Raila kula kiapo

 Raila Odinga, ODM, CORD

Kiongozi wa ODM Raila Odinga akihutubia wafuasi wa chama hicho awali. Picha/MAKTABA 

Na LEONARD ONYANGO

Imepakiwa - Sunday, December 31  2017 at  17:08

Kwa Mukhtasari

KINARA wa muungano wa National Super Alliance (NASA), Raila Odinga amekuwa akikwepa kuapishwa kuwa ‘Rais wa Wawananchi’ licha ya kuwahakikishia wafuasi wake kuwa yuko tayari kula kiapo, Taifa Jumapili imebaini.

 

Mgawanyiko miongoni mwa mawakili wa NASA kuhusu uhalali wa kiapo hicho na shinikizo kutoka kwa mataifa ya kigeni, haswa Amerika, ni miongoni mwa sababu zilizomfanya Bw Odinga kufutilia mbali mpango wake wa kutaka kuapishwa.

Kikosi cha mawakili wa NASA kinachoongozwa na Wakili Paul Mwangi kinamtaka Bw Odinga kutumia mbinu mbadala kushinikiza demokrasia badala ya kuapishwa kuwa rais.

Kulingana na mawakili hao, athari za kujiapisha zitatia doa sifa nzuri ya Bw Odinga humu nchini na kimataifa.
Badala yake, mawakili wa NASA wamemshauri Bw Odinga kutumia ‘Bunge la Wananchi’ kupigania demokrasia na kushinikiza baadhi ya vifungu katika katiba kufanyiwa mabadiliko.

Kwa upande mwingine, kundi la mawakili wanaoongozwa na Dkt Miguna Miguna linataka Bw Odinga aapishwe.

Jumapili iliyopita, Dkt Miguna alidai kuwa alizuiliwa na polisi kwa takribani saa nne baada ya kumshuku kuwa alikuwa akienda kumwapisha Bw Odinga katika hoteli ya Sun N Sand, Kikambala katika Kaunti ya Kilifi ambapo vinara wa NASA walikuwa wakikutana na viongozi kutoka kaunti za Pwani.

“Nilizuiliwa kwa muda wa saa nne na polisi waliokuwa na silaha baada ya kunishuku kwamba nilinuia kumwapisha Bw Odinga kuwa rais. Mbona polisi hawakungojea nimwapishe ndipo wanishike?” akadai Dkt Miguna.

Bw Odinga alilazimika kutoka nje ya kikao hicho mara kwa mara baada ya viongozi wa NASA kutoka Kaunti za Mombasa, Kilifi, Taita Taveta na Kwale kushinikiza aapishwe kabla ya kumalizika kwa kikao hicho.

Katika kikao hicho, mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir alimpa Bw Odinga Biblia na akamtaka aape lakini kinara wa NASA akapuuzilia mbali shinikizo hizo.

“Wanaomsukuma Bw Odinga aapishwe wanataka kutumia njia ya mkato badala ya kutia bidii. Kuna njia nyingi mbadala tunazoweza kutumia kufanikisha malengo yetu,” ikasema taarifa ya ushauri kutoka kwa mawakili wa NASA.

Bw Odinga amejipata katika njiapanda kwani wafuasi wake wamekuwa wakimshinikiza kuapishwa kuwa rais.
Mkuu wa Sheria Githu Muigai wiki iliyopita alishikilia kuwa Bw Odinga atafanya kosa la uhaini ambalo adhabu yake ni kunyongwa ikiwa atajiapisha kuwa rais.

Wakati wa mazishi ya aliyekuwa mbunge wa Kitui Magharibi Francis Nyenze, wiki iliyopita, Bw Odinga alisisitiza kuwa yuko tayari kufa ikiwa kifo chake kitasaidia kupalilia demokrasia nchini. “Ikiwa kifo ndicho kitafanikisha demokrasia basi niko tayari kunyongwa,” Bw Odinga akaambia waombolezaji.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa, matamshi yaliyotolewa na Bw Odinga katika Kaunti ya Kitui yalilenga kuwatia moyo wafuasi wake.

“Ukweli ni kwamba Bw Odinga amelemewa na shinikizo kutoka kwa mataifa ya kigeni na utata wa kisheria kuhusu athari za kujiapisha. Wafuasi wa NASA wamekuwa wakimshutumu kwa kuwa ‘mwoga’. matamshi hayo aliyotoa Kitui yalilenga kuwahakikishia kwamba bado ana mpango wa kujiapisha,” anasema wakili Tom Mboya.

Mbali na utata wa kisheria, Bw Odinga amekuwa akipokea shinikizo kutoka kwa Amerika za kumtaka kutupilia mbali mpango wa kuapishwa.

“Kubuni serikali mbadala haitasaidia na badala yake kutatia doa sifa ambayo umejipatia nchini Kenya na rubaa za kimataifa,” akasema Donald Yamamoto, naibu waziri wa masuala ya Afrika alipokuwa akihutubia wanahabari nchini Amerika.

Bw Yamamoto alisema kuwa alikutana na Bw Odinga na kumhimiza kuhakikisha kuwa analinda sifa yake ya kuwa kiongozi ambaye amejitolea mhanga kupigania demokrasia.

Balozi wa Amerika Bob Godec alikuwa miongoni mwa viongozi wa kwanza kumpongeza Bw Odinga alipofutilia mbali mpango wake wa kuapishwa Desemba 12 uwanjani Jacaranda.

“Kufutiliwa mbali kwa mpango wa kuapishwa ni hatua nzuri na ishara kwamba kuna uwezekano wa kufanya mazungumzo ili kumaliza utata wa kisiasa unaogubika Kenya,” akasema Bw Godec.

Duru ndani ya NASA zinasema kuwa vinara wa muungano huo, Bw Odinga, Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC) na Moses Wetang’ula sasa watatumia Bunge la Wananchi kuhinikiza ajenda yao ya kutaka kufanyia mabadiliko katiba na sheria za uchaguzi.

Muungano wa NASA pia utatumia Bunge la Wananchi kushinikiza kuvunjiliwa mbali kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na kuunda tume mpya itakayoendesha uchaguzi wa 2022.

Mabunge ya kaunti 15 tayari yamepitisha mswada wa kutaka kubuniwa kwa Bunge la Wananchi.

Muungano wa NASA pia unaonekana kulegeza kamba katika kuhimiza wafuasi wake kususia bidhaa na huduma za baadhi ya kampuni zinazohusishwa na Jubilee kama njia mojawapo ya kushinikiza mageuzi.