http://www.swahilihub.com/image/view/-/4294564/medRes/1878612/-/8fqx2bz/-/heda.jpg

 

Miguna Miguna apuuzilia mbali uteuzi awe Naibu Gavana kaunti ya Nairobi

Miguna Miguna

Wakili Miguna Miguna azungumza na mawakili wake na seneta maalumu Judith Pareno Februari 6, 2018 alipofikishwa katika mahakama ya Kajiado siku kadha baada ya kukamatwa nyumbani kwake mtaani Runda. Picha/KANYIRI WAHITO 

Na WYCLIFFE MUIA na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Thursday, May 17  2018 at  13:47

Kwa Muhtasari

Ingawa mawikili Cliff Ombeta na Nelson Havi wa mwanasiasa Miguna Miguna wameelezea matumaini yao kuwa wakili huyo atakubali kuwa Naibu Gavana wa Nairobi, kuna vizuizi ambavyo huenda vikalemeza umoja wao.

 

WAKILI Miguna Miguna ameambia vyombo vya habari hatambui uteuzi awe Naibu wa Gavana Mike Sonko, akiutaja kama hatua ya kukwepa hali halisi.

Pia amefuatisha ujumbe katika ukurasa wake wa Twitter kukataa kuteuliwa kwake.

"Kimsingi ni kwamba vita vya kupiganwa ni sharti kuvishinda. Tulikuwa na ukakamavu Januari 30, 2018, na hamasa imepanda na inalenga ndipo kama mwale. Mambo yanayolenga kutatiza nia halisi hayana maana," ameandika Miguna Miguna.

Ikiwa atakubali, ndoa yake kisiasa na gavana wa Nairobi Mike Sonko na huenda ikakabiliwa na vizingiti kadhaa vya kisheria, kisiasa na kimaadili.

Japo mawikili wa mwanasiasa huyo Cliff Ombeta na Nelson Havi wameelezea matumaini yao kuwa wakili huyo atakubali kuwa Naibu Gavana wa Nairobi, kuna vizuizi ambavyo huenda zikalemeza umoja wao.

Chini ya katiba, Kipengele cha Sita cha Uraia na Uongozi, afisa yeyote wa serikali sharti awe raia wa Kenya.

“Afisa wa serikali au afisa wa jeshi hatakubaliwa kuwa na uraia wa mataifa mawili,” Kipengele cha pili (78) 2 cha Katiba kinanukuu.

Miezi miwili iliyopita serikali ilimfurusha Miguna hadi Canada ambapo ni raia na kutangaza kitambulisho chake cha Kenya kuwa kisichotambulika na serikali.

“Kitambulisho cha Miguna kwa sasa ni stakabadhi batili. Hata kama atapata uraia wake sharti atume maombi ya kitambulisho ili aweze kupata pasipoti,” alisema Katibu katika Idara ya Uhamiaji Gordon Kihalangwa.

Mapema Alhamisi, Spika wa Kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi amethibisha pendekezo la Sonko lakini akasisitiza sharti Miguna apate uraia wa Kenya kabla ya madiwani wa Nairobi kumpiga msasa kama inavyotakikana kisheria.

“Kwa sasa Miguna ni raia wa Canada. Ni sharti asuluhishe utata wa uraia wake na serikali kabla ya bunge la kaunti kumuidhinisha,”alisema Bi Elachi.

Hata hivyo, Miguna ameshikilia kuwa hataomba pasipoti ya Kenya na kusisitiza kuwa yeye ni Mkenya kwa kuzaliwa.

Iwapo Miguna ataondolewa vizingiti vya kisheria, atakabiliwa pia na kibarua kigumu cha kuwashawishi madiwani wa kaunti ya Nairobi kuidhinisha uteuzi wake.

Kaunti ya Nairobi ina madiwani 124 na Miguna atahitaji kuungwa mkono na zaidi ya madiwani 90 ili aweze kuwa naibu gavana.

Hofu

Tayari Spika Elachi na Seneta wa Nairobi Johnston Sakaja wameelezea hofu yao kuhusu uwezekano wa wakili huyo kuidhinishwa na bunge la kaunti.

“Miguna hatakuwa naibu gavana wa Nairobi. Nawahakikishia hilo,”alisema Bw Sakaja.
Kwa upande wake Bi Elachi alimshauri wakili huyo alijitayarishe kwa kampeni kali ya kuwashawishi madiwani kwa sababu wadhifa wa naibu gavana ni wa kisiasa.
Kiongozi wa wengi katika Kaunti ya Nairobi Abdi Guyo jana aliongoza madiwani wa Jubilee kupinga uteuzi huo wakisema Miguna si mwanachama wa chama chao.
Chama cha Jubilee kinaonekana kugawanyika kuhusu uteuzi wa Miguna huku kinara wa walio wengi Bungeni Aden Duale na mwenzake wa Seneti Kipchumba Murkomen wakiunga mkono na kutaka serikali impe wakili huyo pasipoti ili aweze kurejea nchini.
Uteuzi huu vilevile uliwashangaza wengi ikizingatiwa kuwa Sonko na Miguna wana sifa na maadili tofauti kama ardhi na dunia.
Wawili hao wamekuwa wakirushiana cheche kali za maneno na kutofautiana vikali kuhusu uongozi wa jiji la Nairobi.
Mnamo Mei 2016, Sonko alisema licha ya Miguna kumshambulia kila mara, atakapochaguliwa kuwa gavana atampa wadhifa katika serikali yake. Miguna alitumia maneno makali kujibu gavana huyo, “Ndugu yangu Sonko siwezi hudumu chini au pamoja na jambazi na.Unaelewa?” alimuuliza Sonko.
Wakati wa mdahalo wa wawaniaji wa ugavana Nairobi, Miguna aliwakabili vikali Sonko na mtangulizi wake Dkt Evans Kidero kwa kushirikiana na wakora kufuja fedha za kaunti.

Kwa upande wake,Sonko alimjibu Miguna kwa kumtaja kama 'mtu mwenye akili punguani’.

Mnamo Jumatano jioni Bw Mike Mbuvi Sonko ambaye ndiye gavana wa Nairobi alitangaza kumteua Miguna Miguna.

Januari 2018, aliyekuwa naibu wa gavana Nairobi Polycarp Igathe alijiuzulu kwa madai kuwa alishindwa kufanya kazi na Sonko. Siku za hivi karibuni, Gavana huyo amekuwa akituhumiwa kushindwa kudhubiti na kuongoza kaunti ya Nairobi kutokana na uharibifu wa barabara zilizoko jijini, kukithiri kwa wachuuzi ikiwa ni pamoja na kuzidi kwa kiwango cha uchafu.

Hata hivyo, Bw Sonko amemteua Dkt Miguna Miguna kuwa naibu wake kupitia barua iliyotumwa kwa spika wa bunge la kaunti ya Nairobi, Bi Beatrice Elachi.

Kwenye barua yake, gavana huyo alisema Miguna Miguna ambaye ana uraia wa Kenya na Canada, ingawa yuko nchini Canada kwa sasa ameafikia matakwa yote ya wadhifa huo kwa mujibu wa katiba.

"Ninawasilisha jina la Wakili Miguna Miguna kwa bunge la kaunti ya Nairobi apigwe msasa kuwa naibu wa gavana," inasema sehemu ya barua hiyo ambayo Jumatano na Alhamisi imekuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.

Wakenya wameelekeza hisia zao kwenye mitandao ya kijamii, hasa Facebook na Twitter huku wengine wakizua mijadala ya utani. Gabriel Oguda anasema ameshangazwa na wananchi kupongeza hatua ya Sonko kumteua Miguna Miguna kuwa naibu wake, ikikumbukwa kuwa katika uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017 aliwania ugavana Nairobi kama mgombea wa kujitegemea. "Watu wa Nairobi walikataa kumchagua miezi saba iliyopita, ndio hawa sasa wanampongeza Sonko kwa uteuzi wake. Kwani Wakenya huwa wanavuta nini?" akataka kujua Oguda kwenye Twitter.

Kabla ya uchaguzi mkuu, kwenye mjadala wa wawaniaji wa ugavana Nairobi Miguna alionekana kumcharura Sonko na aliyekuwa gavana wa Nairobi Dkt Evans Kidero. Ni kufuatia mjadala huo ambapo Brian Khaniri kwenye Facebook amemuonya gavana Sonko kuwa makini akifanya kazi na jenerali huyo.

"Mike Sonko ajue Miguna Miguna anaweza akamng'atua mamlakani," ametahadharisha

Mnamo Machi 9, kiongozi wa ODM Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta walifanya mkutano wa faragha wa kuleta taifa pamoja. Kamau Maurice anasema 'salamu' za viongozi hao ndizo zimeleta utangamano kati ya Sonko na Miguna. "Uteuzi huo ni nguvu za salamu kati ya Rais na aliyekuwa Waziri Mkuu," anasema Kamau.

Miguna alifurushwa nchini mwezi Machi kwa kuhusishwa na sakata ya kumuapisha Bw Odinga Januari 30 kama Rais wa Wananchi.

Wakili huyo alifaa kurejea nchini Jumatano lakini alifahamisha vyombo vya habari kuwa idara ya uhamiaji haijaanda pasipoti yake.

Titus Nyongesa hata hivyo, anasema idara ya uhamiaji ijue wakili huyo sasa ni 'naibu gavana'.

"Atarejea nchini akiwa ni naibu gavana wala si asiye na utambulisho," aeleza Nyongesa kwenye Twitter.

Mwishoni mwa Machi 2018, kizaazaa kilishuhudiwa katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa JKIA Nairobi ambapo Miguna alizuiwa kuingia Kenya hadi atakapowasilisha pasipoti yake ya Canada kwa wizara ya uhamiaji. Katibu wa kudumu wa wizara ya uhamiaji meja jenerali (mstaafu) Gordon Kihalangwa anasisitiza sharti wakili huyo afuate sheria katika kuomba upya pasipoti ya usafiri.

Licha ya masaibu yanayokumba Bw Miguna, Nelson Havi anampongeza kwa uteuzi huo.

"Hongera kwa kuteuliwa wadhifa huo, mawakala wafisadi Nairobi sasa hawana nafasi," anasema mwananchi huyo.

Jina la Miguna Miguna litapigwa msasa na bunge la kaunti ya Nairobi, na iwapo atapata thuluthi mbili (2/3) ya kura hatakuwa na budi ila kuwa naibu gavana wa kaunti hiyo. Uteuzi wa Sonko umejiri wiki kadha baada ya kaunti ya Nyeri kupitia gavana Mutahi Kahiga kumteua Bi Caroline Karugu kuwa naibu gavana.