Mkurugenzi Mkuu wa Uchumi ang'atuka

Na BERNARDINE MUTANU

Imepakiwa - Wednesday, December 6  2017 at  19:14

Kwa Muhtasari

Mkurugenzi Mkuu wa duka la rejareja la Uchumi Dkt Julius Kipng’etich amejiuzulu. Usimamizi wa duka hilo ulitangaza kujiuzulu kwa Dkt Kipng’etich Jumatano, Desemba 6.

 

Alijiuzulu mwishoni mwa Novemba baada ya kuhudumu humo kwa miaka miwili. Katika taarifa, uchumi ilisema mkurugenzi huyo alijiuzulu kwa lengo la kutimiza mahitaji ya kibinafsi.

Afisa wa Fedha, Bw Mohamed Ahmed Mohamed atakuwa kaimu mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo huku ikitangaza nafasi hiyo.

“Bodi imeanza utaratibu wa kutafuta atakayechukua wadhifa huo, hivi karibuni itamtangaza,” Uchumi ilisema katika taarifa.

Kandarasi ya Dkt Kipng’etich ilikamilika Oktoba baada ya kujiunga na kampuni hiyo Agosti 2015, kutoka Benki ya Equity.

Kabla ya kujiunga na Uchumi, duka hilo lilikuwa chini ya usimamizi wa Bw Jonathan Ciano aliyefutwa kazi pamoja na meneja wengine, huku duka hilo likionekana kuingia katika msururu wa hasara kwa muda wa miaka tatu sasa.

Kufikia sasa duka la Uchumi halifanyi vyema kiuchumi licha ya serikali kulipa mkopo wa kulisaidia kukuza shughuli zake.