http://www.swahilihub.com/image/view/-/3002864/medRes/924657/-/9ds3xez/-/DNKURIAcertifi1107yz.gif

 

Kuria, Kabogo wasema wenyeji Mlima Kenya wanataka maendeleo

Moses Kuria

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria. Picha/MAKTABA 

Na SAMMY WAWERU na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Tuesday, January 8  2019 at  15:01

Kwa Muhtasari

Moses Kuria na William Kabogo wanataka kuona eneo la Mlima Kenya likifaidika kutokana na miradi ya maendeleo.

 

MATAMSHI ya kuonyesha ghadhabu ya Rais Uhuru Kenyatta aliyoyatoa Jumatatu kujibu baadhi ya madai ya viongozi wa eneo la Mlima Kenya waliosema limebaguliwa kimaendeleo, ndiyo gumzo kuu katika mitandao.

Wananchi hasa wa eneo hilo wameelekeza hisia zao katika Facebook na Twitter, wengi wao wakikashifu matamshi ya Rais na kadha wakimuunga mkono.

Baadhi ya viongozi wa eneo la Kati wakiongozwa na mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria wanalalamika Rais Kenyatta ameelekeza maendeleo maeneo mengine ya nchi, na kusahau alikotoka, Kiambu.

Akihutubu mjini Mombasa kiongozi wa taifa alikosoa viongozi hao akishikilia "maendeleo sharti yafanywe kila kona ya nchi ila si anakotoka rais aliye mamlaka au awafanyie maendeleo kwa kuwa ni wetu".

Kenyatta akionekana kuelekezea hamaki zake Moses Kuria alitaka viongozi wanaomkosoa wamkome.

"Kwa hivyo hawa washenzi wawachane na mimi, maendeleo nitayafanya kila sehemu ya nchi," alisema.

Kwenye hotuba yake alikumbusha taifa kuhusu salamu zake za maridhiano na kiongozi wa ODM Raila Odinga za Machi 2018, maarufu handshake, kwamba mojawapo ya ajenda za mkataba ni kufanya maendeleo kila kona ya taifa.

Hata hivyo, Bw Kuria ameshikilia kuwa jimbo la Kati limetengwa kimaendeleo, Rais akiendelea kukuza ngome za upinzani na ambazo hazikumpigia kura kama Mlima Kenya.

"Ndio Rais alikuwa sahihi kuhusu utekelezaji wa maendeleo, lakini ukweli ni kwamba waliomchagua eneo analotoka na jamii ya Mlima Kenya kwa jumla wanalia kupuuzwa," amesema kwenye mahojiano na runinga ya Inooro TV inayopeperusha matangazo yake kwa lugha ya Gikuyu.

Mbunge huyu ambaye kwa sasa katika mitandao anatambulika kama mtetezi wa mwananchi, MK, amesisitiza kuwa eneo la Mlima Kenya halinufaiki kimaendeleo kama maeneo mengine nchini. Kwenye mahojiano hayo ya mapema Jumanne, amesema wakazi wanalia walimpigia kura Rais Kenyatta na Naibu wake Dkt William Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2013 na 2017 kwa wingi, lakini wamebaguliwa.

Kuria alizua malalamishi hayo mara ya kwanza katika mkesha wa kuukaribisha mwaka mpya wa 2019, Desemba 31 ambapo yalipigwa jeki na mbunge wa Bahati, Nakuru, Kimani Ngunjiri. Viongozi kadha wa Kiambu, wakiongozwa na mwakilishi wa wanawake Gathoni Wa Muchomba walikashifu matamshi ya mbunge huyo wakidai alikosea Rais heshima.

Bw Kuria alisuta Kenyatta akieleza maendeleo anayofanya Kiambu ni kutoa vyeti vya waasi wa pombe. Alisema Wa Muchomba na gavana Ferdinand Waititu wanalumbana kuona ni nani aliye na "walevi wengi" ili wapokee ufadhili mkubwa, badala ya kuzindua miradi itakayofaa wakazi wote.

Kabogo

Baada ya mbunge Moses Kuria wa eneo la nyumbani kwa Rais Uhuru Kenyatta ambalo ni Gatundu Kusini kujitokeza kimaosmaso hivi karibuni kulia kwamba Rais Uhuru Kenyatta ametelekeza wajibu wa kutendea haki wenyeji wa Jamii yake kuhusu maendeleo, naye aliyekuwa gavana wa Kiambu, William Kabogo amejiunga na ngoma hiyo.

Huku tayari Bw Kuria akiwa ameshutumiwa  vikali na wandani wa rais kuhusu matamshi yake kuwa “wa Mlima Kenya hutumiwa tu kama mashine ya kujaza kapu la kura lakini hisa za serikali huvunwa faida na maeneo ya upinzani,” amejipata akiomba msamaha lakini anajisahau tena anarudia yayo hayo tu.

Baada ya kuomba msamaha kuwa maneno yake yasichukuliwe kana kwamba alikuwa anamlenga Rais, amebadili misamiati na kutangaza tena kuwa “wanasiasa wote walio nyadhifani eneo la Mlima Kenya wanafaa waelewe kuwa tukiwa ndani ya serikali hii hatujawatendea wenzetu wapiga kura haki yoyote.”

Ameongeza kuwa “sioni ni kwa nini mtu ataamua kunizimba mdomo nisiongee yale ambayo yanakera mtu wa kawaida wa Mlima Kenya, hata huo ukweli uwe mchungu nitausema tu hapa na kwingine…”

Sasa, Kabogo ambaye sadifa  ni kuwa ndiye gavana wa kwanza katika kaunti ya Kiambu ambayo ndiyo ya kuzaliwa ya Rais Kenyatta, akiwa katika mahojiano ya redio na kituo cha Kameme FM, ambacho mmiliki wacho ni Rais na wengine, amesema kuwa “hakuna haja ya kudanganyana.”

Amesema kuwa Rais alitembea kila eneo la Jamii ya Agikuyu akiongea kwa lugha ya mama akiwasihi vijana wasimwangushe.

“Orurire guku Gikuyu-ini guothe akiugaga ndamuthaitha mutikanguithie Jeshi…Akihitaga Ma ya Ngai Mutikananguithie (Alizurura (rais) kila mahali kwetu akisihi vijana wasimwangushe… Akiwarai kwa jina la Mungu kuwa wasimwangushe kwa kura ya 2017,” akasema.

Kabogo alisema kuwa malipo ya kujitoa kama siafu kwenda kupiga kura kumekuwa umasikini, misako ya polisi na mahangaiko ya kila aina nje ya ajira kwa vijana.

“Rais aambiwe kuwa vijana hawajafurahia hata kidogo uongozi wake…hadi sasa tuseme ukweli tu. Na hayo ndiyo yanamkera Bw Kuria kiasi cha kulipuka bila kupenda kwake…ni hali inabidi: Sio kuzuri kamwe,” akasema.

Hata hivyo, Kabogo ameteta kuwa hata viongozi wengine wa Mlima Kenya hawafai kutenganishwa mna kufeli kwa rais katika kutendea mlima Kenya haki.

“Wao ndio wanafaa kumwelezea rais kuhusu hisia za wenyeji. Wale wa maeneo mengine wanapata maendeleo kwa kuwa viongozi wao wamejipanga na wanaongea kwa sauti moja. Hawa wetu hata hawapendani acha tu uwapate wamekaa katika jukwaa moja wakijadiliana kuhusu maendeleo yetu,” akasema.