http://www.swahilihub.com/image/view/-/3002864/medRes/924657/-/9ds3xez/-/DNKURIAcertifi1107yz.gif

 

Moses Kuria ajitetea na kujutia matamshi yake

Moses Kuria

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria. Picha/MAKTABA 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Friday, January 11  2019 at  12:12

Kwa Muhtasari

Katika siku za hivi karibuni joto la kisiasa limeonekana kupanda nchini Kenya.

 

NAIROBI, Kenya

CHAMA tawala cha Jubilee (JP) kimekuwa katika hali ya vuta nikuvute, kufuatia matamshi ya baadhi ya viongozi kwa Rais Uhuru Kenyatta.

Katika harakati za kuukaribisha mwaka wa 2019, Moses Kuria ambaye ni mbunge wa Gatundu Kusini alidai Rais Uhuru Kenyatta amelitelekeza eneo la Mlima Kenya kimaendeleo, na kuegemea ngome za upinzani. Alisema Rais amepuuza eneo hilo, na analotoka ilhali lilimpigia kura kwa wingi.

"Hii mambo kazi yetu ni kupiga kura halafu maendeleo yanaenda kwingine, hii ujinga tuwache," alisema Kuria, akifafanua matamshi hayo kwa lugha asili ya Agikuyu akiyaelekezea Rais Kenyatta.

Matamshi yake yaliyopigwa jeki na mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri, yamemghadhabisha Bw Kenyatta, Jumatatu akiwataja kama "washenzi" na kwamba maendeleo atayafanya katika kila kona ya nchi. Aliomba Rais radhi baada ya mambo kutibuka, kwa kukemewa na viongozi kadha wa Jubilee, akisema matamshi yake yalipokelewa isivyofaa.

Mbunge huyu jana akiomba msamaha kwa mara nyingine kupitia kikao na waandishi wa habari jijini Nairobi, alisema suala hili limevuka mipaka na kuwa la kibinafsi. Alilalamika kuwa wakosoaji wake wanalenga kuleta uhasama kati yake na Rais. "Ninaomba Rais msamaha kwa neno lolote nililomkosea na ujumbe wangu kupokelewa isivyofaa. Pia, ninawaomba wananchi msamaha. Suala hili limevuka mpaka na kuwa la kibinafsi, kupitia mashambulizi ninayopokea. Ninasikitika wakosoaji wangu wanalenga kuleta uhasama kati yangu na Rais," alisema, akionekana kujutia matamshi yake ya awali.

Kuria alisema maisha yake sasa yako katika hali hatari, kufuatia vitisho anavyopokea. "Tayari nimefahamisha mkurugenzi wa jinai, DCI George Kinoti ambaye ameahidi kufanya uchunguzi na kuchukua hatua," alisema.

Kujiuzulu

Tetesi za kutangaza kujiuzulu kwa mbunge huyu zimekuwa zikisambaa kwenye mitandao na baadhi ya vyombo vya habari. Hata hivyo, kwenye mahojiano na runinga ya Citizen baadaye jana jioni, Kuria alisema hayo ni madai potovu yanayosambazwa na vyombo habari bandia.

Kwenye ufafanuzi wake kuhusu matamshi yaliyomtia taabani, na ambao ulionekana kuwa kinaya cha video ya alipozungumza, Kuria alisema aliyaelekeza kwa viongozi wa kaunti ya Kiambu ila si Rais Kenyatta.

"Nililenga uongozi wa Kiambu, hasa gavana na mwakilishi wa wanawake. Niliwasihi wawe wakialika Rais kuzindua miradi kama ujenzi wa barabara lakini su kutoa vyeti vya waasi wa pombe," alieleza.

Ferdinand Waititu ndiye gavana wa Kiambu, naye mwakilishi wa wanawake ni Gathoni Wa Muchomba.

Mbunge huyu pia aliwasuta viongozi wanaomuingilia, akisema katika uchaguzi mkuu wa 2013 na 2017 alikuwa katika mstari wa mbelee Jubilee kupigia debe Rais Kenyatta na Naibu wa Rais William Ruto wachaguliwe katika awamu ya kwanza na ya pili mtawalia.