http://www.swahilihub.com/image/view/-/4137314/medRes/1779193/-/nmfxmbz/-/WW.jpg

 

Muuzaji wa magazeti asimulia alichoshuhudia katika mauaji ya Muchai

Ronald Nyangaresi Siango

Muuzaji Magazeti Ronald Nyangaresi Siango alipotoa ushahidi Oktoba 12, 2017 dhidi ya washukiwa saba waliokanusha kunuua George Muchai. Picha/ RICHARD MUNGUTI 

Na RICHARD MUNGUTI

Imepakiwa - Thursday, October 12  2017 at  21:07

Kwa Mukhtasari

MUUZAJI magazeti Alhamisi  alisimulia jinsi alishuhudia aliyekuwa Mbunge wa Kabete George Muchai akiuawa na jambazi usiku wa manane kwenye barabara ya Kenyatta Avenue miaka miwili iliyopita aliposimama kununua magazeti.

 

Bw Ronald Nyangaresi Siango alisema alikuwa akimwuzia magazeti Muchai kwa muda wa miaka mingi na kwamba usiku wa Februari 6, 2015 ulikuwa tu usiku kama wa siki zingine.

Bw Siango alimweleza Jaji James Wakiaga kwamba mwendazake alisimama karibu na steji iliyo ng’ambo ya jengo la General Post Office (GPO) kuchukua gazeti.

“Gari la Muchai lilisimama kisha nikakimbia kumpa magazeti, mara tu gari jeupe likasimama mbele ya gari la Muchai na kuziba njia,” alisema Bw Siango,

Muuzaji magazeti huyo alisema , “Mwanaume aliyekuwa amejihami kwa bunduki alitoka kwenye gari lililosimama mbele ya gari la Muchai na kuwafyatulia risasi wote-Muchai, walinzi wake wawili na dereva.”

Ufyatuaji wa risasi ulichukua muda mchache kisha jambazi huyo akarudi kwenye gari kisha akachomoka kwa mwendo wa kasi.

“Kufumba na kufumbua macho jambazi alichomoka kutoka kwa gari hilo ndogo jeupe akiwa na bunduki na kuanza kuwamininia risasi Muchai, walinzi na dereva,” alisema muuzaji huyo wa magazeti ya humu nchini na majarida ya nchi za kigeni.

Mahakama iliambiwa kwamba milio mikuu ya risasi aliyosikia ilimtia woga na hata akatoroka.

“Sikumwona sura mwanaume hiyo ambaye alikuwa anawaua Muchai. Aliwamininia risasi Muchai , walinzi wake wawili na dereva kisha akarudi kwa gari na likachomoka mbio.

Shahidi huyo alisema hakuweza kutambua sura ya jambazi huyo.

Bw Siango alisimulia hayo alipotoa ushahidi katika kesi ya mauaji dhidi ya Margaret Wachuiri, Raphael Gachii, almaarufu Butcher Kimani Anyonyi almaarufu Musti, Stephen Lipapo, alias Chokore, Erick Isabwa, almaarufu chairman, Jane Kamau, almaarufuas Shiro, na Simon Gichamba.

Kesi itaendelea Desemba 13, 2017.