http://www.swahilihub.com/image/view/-/3221352/medRes/877790/-/u7i08t/-/DNCOASTKWALE2209C.jpg

 

Mvurya, naibu waambia wenyeji sababu ya kutoka ODM

Gavana wa Kwale, Salim Mvurya

Gavana wa kaunti ya Kwale, Salim Mvurya. Picha/KEVIN ODIT  

Na WINNIE ATIENO

Imepakiwa - Sunday, January 8   2017 at  14:32

Kwa Mukhtasari

Gavana Salim Mvurya na naibu wake Fatuma Achani wamewaelezea wakazi wa kaunti ya Kwale sababu ya kukihama chama cha ODM na kukumbatia Jubilee.

 

GAVANA Salim Mvurya na naibu wake Fatuma Achani wamewaelezea wakazi wa kaunti ya Kwale sababu ya kukihama chama cha ODM na kukumbatia Jubilee

Bw Mvurya amesema wanaomwonea wivu wanampaka tope wakidai alipeana leseni ya uchimbaji wa madini eneo la Mrima.

Aidha, amewataka wakazi kutoangalia kabila lake bali kumpigia kura sababu ya utendakazi wake.

“Mimi naomba tu kura zenu ili niendeleze miradi yangu ya elimu na afya bora,” akasema.

Wakiongea kwenye halfa ya kuwapa wanafunzi fedha za elimu, aidha Bw Mvurya alisema kwa mara ya kwanza, wanafunzi wengi wa kaunti hiyo wanafanikiwa kusoma hadi vyuo vikuu sababu ya uongozi wake.

“Gavana Mvurya amefanya kushinda viongozi wengine ambao waliwahi kuwa hapa miaka 50 iliyopita. Desturi ya viongozi wetu walikuwa wakisema shamba liende linaenda,” akasema Bi Achani.

Bi Achani aliwataka wakazi kuwa makini na viongozi wengine ambao aliwataja kuwa wabinafsi.

Achani alisema viongozi wa ODM wamekuwa wakimtukana Mvurya sababu alikihama chama hicho.

Kustahimili matusi

Alisema gavana amestahimili matusi na kejeli tangu mwaka wa 2013.

“Amestahimili matusi na kejeli zote. Aliambiwa atafute gari nzuri eti kiongozi wa chama anakuja... Maskini gavana wenu si tajiri lakini tukatafuta gari katika uwanja mdogo wa ndege. Alipofika kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, aliacha gari letu na kulipanda gari la Bw Joho. Si madharau hayo?” akauliza Bi Achani.

Amesema kuna watu wanazunguka na vijikaratasi wakidai kuwa gavana huyo amepeana leseni madini yachimbwe.

“Wale wanaozunguka na vijikaratasi ni vibaraka wa ndugu zetu wa Mombasa. Gavana wa Mombasa aliapa atahakikisha atatafuta pesa zote hadi pale atakapohakikisha anammtoa Bw Mvura uongozini,” akadai Bi Achani.

Aliwaonya wakazi wa Kwale kuwa Bw Mvurya akiondoka mamlakani miradi ya Bw Mvurya itasimama hususan ya elimu na afya bora.

Bi Achani alisema chuki dhidi ya Bw Mvurya pia ilitokana na sababu zake za kusimamisha uchimbaji wa madini eneo la Mrima.

“Madini hapo yana miale ya simu, hawa wakazi wa Mrima watapelekwa wapi? Ndio maana gavana wetu akapinga,” akaeleza.

Aliwarai wakazi kumpigia kura Bw Mvurya kupitia chama cha Jubilee.

Alipoenda Jubilee alikaribishwa vizuri sana.