Mwanamke awasilisha kesi kusimamisha mazishi ya Too

Mark Too

Mbunge wa zamani Bw Mark Too. Picha/MAKTABA 

Na RICHARD MUNGUTI

Imepakiwa - Wednesday, January 4  2017 at  18:02

Kwa Mukhtasari

MWANAMKE anayedai walijaliwa kumpata mtoto wa kiume na aliyekuwa mbunge maalum na mfuasi sugu wa chama cha KANU Mark Too miaka 16 iliyopita amewasilisha kesi ya kusimamisha mazishi yake Jumatatu.

 

Bi Fatuma Ramadhan Hassan anaomba Mahakama kuu ishurutishe wajane wawili wa Mark Too wasimzike mume wao hadi hatma ya mwana waliyemzaa na marehemu ijulikane.

Mwanamke huyo anadai kwamba marehemu alikuwa anamlipia karo mwanawe na “vile sasa ameaga elimu na maisha ya baadaye ya mtoto huyo yanagubikwa na wingu jeusi.”

“Hakuna mtu sasa atakayetambua hatma ya mtoto tuliyemzaa na Mark ,” anasema Fatuma katika ushahidi aliowasilisha mbele ya Jaji Aggrey Muchelule aliyeiratibisha kesi hiyo kuwa ya dharura.

Fatuma amefichua walikuwa marafiki na marehemu punde tu alipotalikiwa na mumewe Mohammed Bakari mnamo 1999 ndipo walimzaa mvulana huyo aliye na miaka 16 sasa.

“Tulipotengana na aliyekuwa mume wangu Mohammed Bakari tulifanya urafiki na marehemu na mnamo Machi 16, 2000 tulibarikiwa na mtoto wa kiume,” akafichua.

“Bila shaka hakuna shaka yoyote, marehemu ndiye baba wa kibayolojia wa mwanangu,” anasema Fatuma katika ushahidi aliowasilisha kortini kupitia kwa wakili Danstan Omar .

Mlalamishi huyo anasema endapo mazishi yatafanywa bila kumshirikisha mwanawe itakuwa ni dhuluma na mateso makubwa ya kimawazo.

Bw Omari alimweleza Jaji Muchelule kwamba mahakama ya kuamua kesi za watoto ilikuwa imemwamuru marehemu awe akimlipia karo mtoto huyo waliyemzaa pamoja.

Jaji Muchelule aliyeratibisha kesi hiyo kuwa ya dharura na kuamuru isikizwe Januari 6 alielezwa kwamba mvulana huyo anataka kushiriki katika mipango ya mazishi ya baba yake Mark Too.

Kutoshirikishwa

Fatuma amewashtaki wajane wawili wa marehemu Bi Sofi Too na Mary Too aliosema “hawajamshirikisha katika mipango ya mazishi.”

Pia amekishtaki chumba cha kuhifadhia maiti cha Lee. 

Too alifariki Desemba 31, 2016 na mwili wake umehifadhiwa katika chumba cha Lee Funeral Home Nairobi.

Mahakama imeelezwa ikiwa mtoto huyo hatakubaliwa kushiriki katika mazishi hayo “ataumia kimawazo na hata sasa anahitaji kushauriwa na mtaalamu.”

“Shule zinafunguliwa leo(jana) na hakuna mawasiliano yoyote kuhusu karo yake kutoka kwa upande wa baba yake,” anasema Fatuma huku akiomba , “Chumba cha kuhifadhi maiti cha Lee kisipeane mwili wa marehemu ukazikwe kabla ya kesi aliyoshtaki kusikizwa na kuamuliwa.”

Mama huyo anaomba mahakama kuu iamuru wajane hao wa marehemu wampe kiwango kikubwa cha pesa za kugharamia karo ya mwanawe mwanasiasa  huyo mashuhuri.

Pia anaomba wajane hao waamriwe wasimbague mwanawe mbali ashirikishwe katika mipango yote ya mazishi.

Jaji Muchelule alielezwa kuwa mahakama inayoshughulikia kesi za watoto ilikuwa imemwamuru Bw Too awe akilipa karo ya mwanawe.

Kesi hiyo itasikizwa Ijumaa.