http://www.swahilihub.com/image/view/-/2412312/medRes/804970/-/10ai54jz/-/dnMurang%2527agovernor3108.jpg

 

Mwangi Wa Iria atengea barabara za mashinani Sh400 milioni

Mwangi wa Iria

Gavana wa Murang'a Mwangi wa Iria akihutubia wanahabari awali. Picha/JOSEPH KANYI 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Thursday, January 10  2019 at  13:06

Kwa Muhtasari

Hii ni awamu ya tatu ya mpango wa kukarabati barabara.

 

MURANG'A, Kenya

GAVANA wa Murang’a,Mwangi Wa Iria ametangaza kutengea barabara za mashinani katika wadi zote 35 kitita cha Sh400 milioni za ukarabati.

Alisema kuwa hii ni awamu ya tatu ya mpango huo ambao awamu ya kwanza alitenga Sh1.0 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2015/16 na kisha kiwango sawa mwaka wa kifedha wa 2016/17 na ambapo sasa ndiye huyo na bajeti mpya.

Akiwa afisini mwake Jumatano na wadau katika sekta ya uchukuzi, alisema kuwa changamoto zile kaunti imekuwa ikikumbana nazo katika ukarabati wa barabara hizo za mashinani ni pamoja na bajeti finyu kutokana na uhaba wa pesa.

“Tukome kuelezana yale tu ya uongo... Tuna shida kuu kuhusu jinsi serikali kuu husambaza pesa mashinani. Kunatokea mara kwa mara ucheleweshaji ambao haueleweki, zikiingia tunajipata tuko na bili za dharura na tunavurugika katika bajeti,” akasema.

Hata hivyo, alisema kuwa ikiwa barabara hizo zitakarabatiwa kama ilivyo katika ratiba ya utekelezaji, basi atahakikisha kuwa kabla ya kung'atuka uongozini mwaka wa 2022, atakuwa ameafikia asilimia 90 ya barabara zote mashinani kuwa za kuafikika katika kila aina ya msimu.

“Kunyeshe au kusinyeshe, barabara hizo zitakuwa zinaafikiwa na uchukuzi mwafaka katika kila eneo. Hakuna mkulima nataka kusikia akilalamika kuwa mavuno yake yaliharibikia barabarani kwa kukosa mbinu ya uchukuzi kufuatia barabara mbovu,” akasema.

Alisema kuwa wengine ambao huumia zaidi katika hali ya barabara mbovu ni wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ambao husafiri kurefu kufika shuleni mwao.

Pia, alisema kukarabatiwa kwa barabara za mashinani katika Kaunti hiyo kutazidisha pato kwa kilimo kwa zaidi ya asilimia 40 kufuatia kuafikika kwa biashara kati ya wateja na wakulima nje ya lango bomani badala ya kusafiri hadi sokoni.