http://www.swahilihub.com/image/view/-/4802912/medRes/2138593/-/rcqe4u/-/wangari.jpg

 

Mwaniki avalia nyunga maslahi ya wakulima wa majanichai na kahawa Murang'a

Mbunge wa Kigumo, Wangari Mwaniki  

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Friday, October 12  2018 at  12:56

Kwa Muhtasari

Viongozi waliochaguliwa katika viwanda ndio wanakandamiza wakulima kwa kufuja pesa


 

Murang'a. Baadhi ya wabunge kutoka Murang'a wamemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati na kunusuru wakulima wa majanichai na kahawa kutokana na bei duni.

Wameteta kwamba wakulima wake wanaendelea kupata hasara ikilinganishwa na gharama ya ukuzaji wanayotumia. Wakiongozwa na mbunge wa Kigumo Wangari Mwaniki Alhamisi, walimtaka Rais Kenyatta kutatua shida inayowafika wakulima hao.

"Tunaomba Rais utusaidie kutatua shida za wakulima wa majanichai na kahawa kwa sababu ya bei yake duni. Wakulima wanatumia pesa nyingi kukuza mazao haya," alisema Wangari akihutubu katika ibada ya mazishi ya mwanamuziki wa nyimbo za Agikuyu na benga Joseph Kamaru.

Mbunge huyu alisema wakulima wanang'oa mimea ya majanichai na kahawa kwa sababu ya kupata hasara inayotokana na bei duni ya mazao. Alieleza kwamba matumaini ya wakulima wa majanichai na kahawa sasa yako mikononi mwa Rais Kenyatta aliye na mamlaka kuamuru halmashauri na bodi zinazonunua mazao yao kuwalipa bei nafuu.

Hata hivyo, wakulima wa mazao hayo wanalalamika kuwa viongozi waliochaguliwa katika viwanda ndio wanakandamiza wakulima kwa kufuja pesa. Awali John Karanja mkulima wa majanichai na kahawa Murang'a alizungumza na Swahili Hub kuwa malipo ya kila mwaka ya ziada ya majanichai, mwaka 2018 yamepungua yakilinganishwa na miaka mingine. "Bei tunayolipwa kwa kilo ni ishara ya kukata wakulima mikono kabisa, ile ya juu tumewahi kulipwa ni Sh50 kwa kilo. Tunashangaa kwa nini malipo ya ziada 2018 yakawa Sh42 kwa kilo, hii ni bei ya chini ilhali tuliambiwa yalinunuliwa vizuri sokoni," alisema Karanja.

Mbali na Murang'a, maeneo mengine yanayokuza majanichai ni; Kericho, Bomet, Nandi, Kiambu na Kisii. Pia kaunti za Nyamira, Meru, Nyeri, Kirinyaga, Embu, Kakamega na Nakuru hukuza zao hilo.

Bw Apollo Maina alisema kwamba malipo ya kila mwezi kilo huwa Sh15. Majani ya chai huchumwa kila siku, na kwamba hushurutika kuajiri wafanyakazi.
"Kwa siku kupata kilo 20 kwa kila mfanyakazi ni vigumu, humlipa Sh300. Ni wazi malipo ninayopokea huishia kwa wafanyakazi," alieleza.

Ibrahim Maina, mkulima wa mimea hiyo alisema anaikuza kwa minajili ya kukimu familia yake kwa kuwa bei yake ni ya chini mno kiasi cha kutomuwezesha kufanya maendeleo yoyote.