Mzazi azirai baada ya kuambiwa alipe karo ya Sh16,000

Na  FADHILI FREDRICK na BENSON MATHEKA

Imepakiwa - Thursday, January 11  2018 at  21:17

Kwa Mukhtasari

KULIKUWA na kizaazaa katika shule ya upili ya wasichana ya Kingwede, kaunti ya Kwale, mzazi alipoanguka na kuzirai baada ya kutakiwa kulipa karo.

 

Bw Ndaikwa Chale kutoka wilaya ya Kinango alikuwa amempeleka binti yake kujiunga na Kidato cha Kwanza katika shule hiyo alipoanguka na kuzirai.

Inasemekana alishtuka alipotakiwa kulipa karo ilhali hakuwa na pesa za kutosha.

Binti yake Fatuma Chale, 16, alipata alama 319 kati ya 500 kwenye mtihani wa darasa la nane (KCPE), mwaka jana licha ya kutoka familia maskini na kuitwa kujiunga na shule hiyo.

Kulingana na msichana huyo, baba yake alikuwa amenunua vifaa vilivyohitajika shuleni na akabaki na Sh800 pekee ambazo alidhani zilitosha kulipa karo yote.

“Tulikuwa tumenunua vitu vilivyohitajika shuleni kabla ya kufika shuleni alasiri lakini baba yangu alipoambiwa kwamba alitakiwa kulipa karo, alianguka na kuanza kuhara na kutapika,” alisema msichana huyo.

Alisema wazazi wake wawili huwa wanauza makaa na hawawezi kupata Sh16,993 walizotakiwa kulipa karo.

Mwalimu Mkuu wa shule ya wasichana ya Kingwede Bi Peninah Mwinyi alisema wawili hao waliwasili shuleni alasiri wakionekana wachovu.

“Kuna mzazi aliyefika akiandamana na binti yake na kuelekea kusajiliwa lakini alipotakiwa kulipa karo ya shule, alizirai,” alisema Bi Mwinyi.

Mwalimu huyo alisema alishuku kushindwa kupata karo ya shule ya binti yake kulimuathiri mwalimu huyo kisaikolojia.

“Tulimkimbiza katika hospitali ya kaunti ya Msambweni na tukawasiliana na jamaa zake,” alisema Bi Mwinyi.

Wazazi wengi wamekuwa wakilalamika kuwa huenda watoto wao wakakosa nafasi katika shule za upili kwa kukosa karo licha ya serikali kutangaza elimu bila malipo katika shule za upili za kusoma na kurudi nyumbani.

Serikali imeonya walimu wakuu dhidi ya kuwatoza wazazi ada zozote katika shule hizo na kuwataka kufuata mwongozo wa karo uliotolewa na wizara ya elimu.

Karo ya shule za kitaifa ni Sh53, 554 kwa mwaka baada ya serikali kulipa Sh22,244, shule za mkoa ni Sh40,535 kwa mwaka.