Mzee wa miaka 70 ajiua kwa kutorokwa na mke wa pili

Na BARACK ODUOR

Imepakiwa - Thursday, December 7  2017 at  15:35

Kwa Muhtasari

MWANAMUME wa umri wa miaka 70 alijitoa uhai katika Kaunti ya Homa Bay baada ya kuachwa na mkewe.

 

Bw Samuel Oloto Onjoga, kutoka kijiji cha Kauma, kaunti ndogo ya Kabondo Kasipul, alijiua Jumanne jioni baada ya mke wake wa pili kutoroka nyumbani katika hali isiyoeleweka.

Chifu wa eneo hilo, Bw Joseph Ndege, aliwaambia wanahabari kwamba, Bw Onjoga alijitia kitanzi kwa kutumia kamba ya mkonge kwenye mwembe ulioko nyumbani kwake.

“Tulimpata akining’inia kwenye mwembe ulio kando ya nyumba yake. Alitumia kamba ya mkonge kujinyonga,” akasema Bw Ndege.

Kulingana na chifu huyo, mke wa pili wa marehemu alitoroka akaenda kuishi katika soko lililo karibu na kumwacha mpweke na mwenye huzuni tele.

“Mzee huyo alikuwa na upweke baada ya mke wake wa pili kumtoroka na kwenda kukodisha nyumba katika soko lililo karibu baada ya kuzozana,” akasema.

Kulingana na wanakijiji, mke wa kwanza wa marehemu alifariki miaka mitano iliyopita. Alipata jiko jipya miaka miwili iliyopita.

Wanakijiji walisema huenda mfanyabiashara huyo wa mifugo alipatwa na matatizo ya kimawazo kwa kuishi peke yake nyumbani, ilhali alikuwa pia na matatizo ya kiafya.

Kamanda wa polisi wa Kaunti ya Homa Bay, Bw Marius Tum, alisema polisi wa kaunti ndogo ya Rachuonyo Mashariki wameanzisha upelelezi kubainisha ukweli kuhusu kifo hicho.

“Tumeambiwa amekuwa akipitia hali ngumu kimaisha tangu mke wake alipoaga dunia miaka mitano iliyopita na familia yake inashuku huenda hilo pia lilichangia uamuzi wake kujitia kitanzi,” akasema Bw Tum.

Mwili wake ulihamishwa hadi katika mochari ya hospitali ya kaunti ndogo ya Rachuonyo kusubiri kufanyiwa upasuaji wa kubainisha chanzo cha kifo.

Kumekuwa na matukio mengi ambapo jamaa huhama katika boma zao na kuamua kwenda kuishi katika masoko yaliyo karibu na eneo hilo.