Timamy: NLC iwafidie walioathirika mradi wa makaa ya mawe

Issa Timamy na Profesa Muhammad Swazuri

Gavana wa Lamu, Issa Timamy (kulia) na Mwenyekiti wa NLC, Profesa Muhammad Swazuri wakati Swazuri alipowasili Lamu kuzindua shughuli ya ukaguzi na uidhinishaji wa majina ya waathiriwa wa mradi wa nishati ya makaa ya mawe huko Kwasasi, Lamu mapema Februari. Gavana Timamy ameionya NLC dhidi ya  kukiuka matakwa na kuwadhulumu wamiliki wa ardhi zilizotwaliwa kufanikisha ujenzi wa mradi huo. Picha/KALUME KAZUNGU 

Na KALUME KAZUNGU

Imepakiwa - Friday, February 17  2017 at  15:44

Kwa Mukhtasari

Serikali ya Kaunti ya Lamu imeionya Tume ya Kitaifa ya Ardhi nchini (NLC) dhidi ya kukiuka matakwa na kuwadhulumu haki ya fidia waathiriwa ambao ardhi zao zilitwaliwa kufanikisha ujenzi wa mradi wa nishati ya makaa ya mawe.

 

SERIKALI ya Kaunti ya Lamu imeionya Tume ya Kitaifa ya Ardhi nchini (NLC) dhidi ya kukiuka matakwa na kuwadhulumu haki ya fidia waathiriwa ambao ardhi zao zilitwaliwa kufanikisha ujenzi wa mradi wa nishati ya makaa ya mawe.

NLC tayari imeanzisha shughuli ya kuwakagua na kuwaidhinisha wamiliki wa ardhi hizo kijijini Kwasasi, Kaunti ya Lamu.

Alhamisi, akizungumza na wanahabari mjini Lamu, Gavana wa eneo hilo, Dkt Issa Timamy, aliitaka NLC kutekeleza shughuli hiyo kwa njia ya wazi na haki.

Dkt Timamy alisema tayari amepokea malalamishi kutoka kwa baadhi ya waathiriwa wanaodai kiwango cha ardhi iliyotwaliwa ni kikubwa ikilinganishwa na fedha wanazopaswa kufidiwa.

Kila ekari ya ardhi iliyotwaliwa kwa ujenzi wa mradi huo wa nishati ya makaa ilikadiriwa na kupasishwa kufidiwa Sh800,000.

Alisema kuna haja ya NLC kuihusisha kikamilifu serikali ya kaunti ya Lamu katika shughuli zote  zinazohusu kuwatambua, kuwakagua na kuwaidhinisha wamiliki halisi wa ardhi za Kwasasi kabla ya shughuli ya kuwafidia waathiriwa hao kutekelezwa.

Aliahidi kusimama na wananchi wake na kuhakikisha kila mmiliki halisi wa ardhi za Kwasasi anapata haki yake ya fidia.

“Ninafahamu kwamba NLC imeanzisha zoezi la ukaguzi na uidhinishaji wa waathiriwa kijijini Kwasasi. Ninaiambia NLC ihakikishe haki inatendeka kwa waathiriwa wote. Tayari nimepokea malalamishi kutoka kwa baadhi ya watu wangu wakidai ardhi iliyotwaliwa ni kubwa mno ikilinganishwa na fedha wanazostahili kufidiwa. Nangoja ripoti rasmi kutoka kwa NLC kabla ya kutangaza msimamo wangu juu ya suala hilo,” akasema Dkt Timamy.

Kwa upande wake aidha, Mwenyekiti wa NLC, Profesa Muhammad Swazuri, alisisitiza kuwa shughuli iiliyoanzishwa na tume yake ya kuwakagua na kuwaidhinisha waathiriwa wa mradi inalenga kuwafurusha wamiliki bandia wa ardhi za Kwasasi.

“Tumepokea majina 615 ya waliowasilisha maombi kwa tume wakidai fidia ya ardhi wanazomiliki Kwasasi. Tunatekeleza ukaguzi na uidhinishaji ili kuhakikisha wamiliki halisi pekee wa ardhi za Kwasasi ndio watakaofidiwa ilhali wale ghushi tutawatema  orodhani,” akasema Profesa Swazuri

Mradi huo unaokadiriwa kugharimu kima cha Sh 200 bilioni uko chini ya usimamizi wa kampuni ya kibinafsi ya Amu Power.

Jumla ya ekari 975 za ardhi tayari zimetengwa katika eneo la Kwasasi ili kufanikisha ujenzi wa  mradi huo unaotarajiwa kuzalisha takriban megawati 1,050 za nguvu za umeme punde utakapokamilika.