NTSA: 'Vuta pumzi' imesaidia kupunguza ajali

Mkurugenzi Mkuu NTSA Francis Meja

Mkurugenzi Mkuu NTSA Francis Meja akihutubia wanahabari awali. Picha/SALATON NJAU 

Na BERNARDINE MUTANU

Imepakiwa - Thursday, April 20  2017 at  12:42

Kwa Mukhtasari

RIPOTI za hivi punde zinaonyesha kuwa visa vya ajali vimepungua kwa kiwango kikubwa kutoka 2016.

 

Katika ripoti ya Mamlaka ya Uchukuzi na Usalama (NTSA) idadi ya waliofariki kutoka Januari 1 hadi Aprili 18, 2017 ilipungua kwa asilimia 9 ikilinganishwa na muda kama huo mwaka 2016.

Ripoti hiyo imeonyesha kuwa watu 898 wamepoteza maisha yao katika kipindi hicho wakilinganishwa na watu 981 wakati huo 2016.

Waliopata majeraha makubwa wakitembea barabarani waliripotiwa kuwa 239 mwaka huu kutoka 358 kutoka Januari 1, hadi Aprili 2016.

Madereva 91 waliripotiwa kufariki muda huo na wengine 149 walijeruhiwa vibaya wakilinganishwa na madereva 117 na 176 kwa mfuatano huo.

Abiria 199 wamefariki na wengine 590 wamejeruhiwa wakilinganishwa na abiria 210 na 696 katika muda huo.

Idadi ya waendeshaji pikipiki ilipungua hadi 165 kutoka 170 mwaka wa 2017 katika muda huo.

Ingawa takwimu hizo zinavutia, NTSA ilishtakiwa dhidi ya matumizi ya kifaa cha kupima viwango vya pombe mwilini (alcoblow).

Hata hivyo, shirika hilo limesisitiza kuwa litaendelea kutumia kifaa hicho kutokana na kuwa kimesaidia kupunguza idadi ya wanaondesha magari wakiwa walevi.