http://www.swahilihub.com/image/view/-/3079834/medRes/1257969/-/gig7eaz/-/jide.jpg

 

Nafasi ya Sanaa katika harakati za kukuza uchumi

Judith Wambura Mbibo

Msanii wa Bongo, Judith Wambura Mbibo 'Jide'. Picha/HISANI 

Na BARAZA LA SANAA LA TAIFA (TANZANIA)

Imepakiwa - Wednesday, November 16  2016 at  16:06

Kwa Mukhtasari

BARAZA la Sanaa la Taifa (Basata) ni asasi ya Serikali iliyoanzishwa mwaka 1984 kwa lengo la kukuza, kuendeleza na kuraghibisha maendeleo ya sanaa hapa nchini.

 

Maelezo mafupi yanatolewa kuhusu shughuli zake kama ifuatavyo:

Neno msanii linatafsiriwa  katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu kama mtu mwenye ustadi wa kuchora, kuchonga au kutia nakshi. Vilevile linafsiriwa kama mtu mwenye ufundi wa kuunga na kutoa mawazo yake kama vile ushairi au tamthilia, yenye kumvuta msomaji. Kimsingi mtu anayefanya  kazi za sanaa huitwa msanii.

Hivyo sanaa ni nguzo mojawapo ya utamaduni ambayo imejikita katika ubunifu wa mtu binafsi, ujuzi na kipaji, kama talanta aliyopewa na Mwenyezi Mungu.

Hata hivyo wataalamu wengi wa anthropolojia na utamadumi wanasema kuwa  ubunifu ni uwezo alio nao kila binadamu. Kwa mujibu wa Sheria No 23 ya mwaka 1984 Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limeainisha sanaa katika shughuli mbalimbali za ubunifu kama vile uchoraji, uchongaji, uhunzi, ususi, ufumaji, ushonaji, majengo na pia mapishi. Pia tamthilia, filamu, muziki wa dansi, kwaya, taarabu, muziki wa asili, muziki wa mapipa, sarakasi na ngoma.

Shughuli  zote hizi ni baadhi ya kazi zifanywazo na wasanii  kwa malipo iwe kwenye vikundi, vyama, kampuni, serikalini au kwa mtu binafsi.

Sanaa na uchumi vimekuwa  vikiishi pamoja  kwa karne nyingi tangu binadamu alipoanza kuishi duniani. Tafiti za maandiko ya kale zinaeleza wazi kwamba katika mfumo wa maisha duniani ilitangulia sanaa halafu uchumi ukafuatia.

Sanaa imedumu tangu binadamu alipoanza kuishi  kwa sababu msanii alizaliwa. Hivyo sanaa ina historia ndefu  katika nchi yetu. Uumbaji wa dunia na vitu vyote vilivyomo ni kielelezo cha sanaa, Aidha, uumbaji wa binadamu unadhihirisha kuwa Mungu ni msanii wa kwanza. Sanaa hii imeendelezwa na wasanii.

Wasanii wameshiriki kutoa mchango mkubwa katika kuleta maendeleo. Mathalan sanaa ya ngoma imekuwa ikitumika  kukusanya watu kwenye mikusanyiko ya kijamiii, wakati wa kampeni za uchaguzi. Wanasiasa huwatumia wasanii kuwahamasisha watu kuhudhuria kwenye mikutano  na kuhakikisha ujumbe unawafikia.

Aidha kwenye maadhimisho na kampeni mbalimbali za afya, wasanii hutumika kufikisha ujumbe. Ni kutokana na mifano ya fani mbalimbali zilizomo  katika sanaa  tunakubaliana na usemi kuwa sanaa ni tasnia mojawapo yenye uwezo wa kuleta ajira na faida ya kipato kwa mtu binafsi, jamii na taifa kwa jumla. Sanaa pia ina uwezo mkubwa wa kuvutia wawekezaji wa ndani na nje na hivyo kusaidia kuongeza kipato kwa msanii binafsi na taifa kwa jumla.

Nyenzo ya maendeleo

Hivyo sanaa ni nyenzo muhimu ya maendeleo na inaweza kuhamasisha jamii kuondokana na umaskini kupitia aina mbalibali za sanaa, kuvutia kwa watalii na pia ongezeko la utalii na malipo ya kodi kuongezeka.  

Wasanii wengi kwa juhudi zao wamejijengea umaarufu na kujipatia kipato kikubwa. Kwa mfano wako wasanii maarufu kama Steven Jacob (JB), Naseeb Abdul (Diamond Plutinumz), Profesa Elias Jengo, Profesa Mlama, Lady Jay Dee, nk.

Sanaa hufanya mambo mengi makubwa ambayo hueleza juhudi inayofanywa na jamii ya watu, hueleza matatizo katika jamii  na mwisho jamii hutumika kuhifadhi na kuwasilisha kumbukumbu za mambo muhimu katika maisha yao.

Utafiti uliofanywa na Basata uliangalia mchango wa sanaa katika ajira, kuongeza kipato, kupunguza umaskini umetoa taswira  kwamba sanaa bado inatazamwa na watu wengi kama sehemu ya utamaduni na burudani na siyo chanzo cha ajira na kipato.

Tanzania iko katika mchakato  wa kufanya sekta ya sanaa kuwa ni sekta rasmi. Mchakato huu unakumbana na vikwazo kadhaa kama vie mitazamo hasi ya jamii ya kufafanua sanaa kuwa ni burudani tu.

Kwa upande mwingine wako wasanii na wadau wa sanaa wasiotaka kusajiliwa na kuwa chombo rasmi cha kuleta maendeleo ya kiuchumi katika jamii.