http://www.swahilihub.com/image/view/-/2896474/medRes/1136419/-/k85quo/-/MURRAILA2907vg.gif

 

Nasa sasa yasaka uwanja wa kiapo

Kinara wa NASA Bw Raila Odinga akiwa na msemaji wake Bw Salim Lone. Picha/JENNIFER MUIRURI 

Na VALENTINE OBARA

Imepakiwa - Thursday, December 7  2017 at  15:31

Kwa Muhtasari

HALI ya sintofahamu imeibuka kuhusu eneo ambako kinara wa muungano wa NASA, Bw Raila Odinga, ataapishwa Jumanne ijayo kuwa 'Rais wa Wananchi’.

 

Muungano huo umetuma barua kwa kaunti zote zilizopitisha Mswada wa kuunda Bunge la Wananchi kuomba eneo la kumwapisha kiongozi huyo wa Chama cha ODM.

Kamati Andalizi ya Bunge la Wananchi

Barua hizo zilizofichuliwa jana zilitumwa kutoka kwa Kamati Andalizi ya Bunge la Wananchi, ambayo ina wanachama saba, akiwemo mshauri wa NASA, Dkt David Ndii. Ilisemekana agizo hilo lilitoka kwa Bw Odinga.

“Kutokana na kwamba kaunti yako ilipitisha Mswada wa Bunge la Wananchi, wanakamati wa kuandaa kuapishwa kwa rais wanaomba afisi yako itenge eneo katika kaunti yako la kufanyia hafla hii yenye umuhimu mkubwa Desemba 12, 2017,” inasema sehemu ya barua hiyo.

Miongoni mwa kaunti zilizotumiwa barua hiyo ni Kitui, Kisumu, Mombasa na Kakamega.

Kaunti zingine ambazo zimepitisha Mswada huo kufikia sasa ni Homa Bay, Migori, Siaya, Makueni, Vihiga, Busia, Kwale, Kilifi na Mombasa.

Ghasia

Kuna hofu huenda ghasia zikatokea endapo NASA itatekeleza hatua ya kumwapisha Bw Odinga kuwa rais kinyume na katiba, hasa ikizingatiwa kwamba kuna uwezekano serikali itazima majaribio ya kuandaa mkutano wa aina hiyo.

Hata hivyo, Bw Salim Lone, ambaye ni mshauri wa Bw Odinga, Jumatano alipuuzilia mbali wanaosema NASA itasababisha mgawanyiko nchini.

Alisema hafla hiyo itafanywa kwa msingi wa sheria, ingawa hakufafanua zipi.

Kulingana na Bw Lone, kinara huyo wa NASA yuko tayari kwa mashauriano wakati wowote, mradi tu yawe kati yake na Rais Kenyatta na kuwe na ajenda zitakazokubalika kabla mkutano huo, ikiwemo kuhusu haki za uchaguzi.

Kwenye taarifa kwa vyumba vya habari, Bw Lone alisema nchi imegawanyika zaidi kutokana na jinsi uchaguzi wa urais ulivyosimamiwa Agosti 8 na baadaye ule wa marudio Oktoba 26.

Analaumu serikali ya Jubilee kwa kutochukua hatua yoyote kutuliza taharuki ya kisiasa iliyotanda katika kipindi hicho na badala yake kutumia polisi kukandamiza Upinzani. “Uapishaji wa Bw Odinga utafuata sheria. Utasaidia kuzuia mgawanyiko zaidi kwa kuwapa Wakenya matumaini ya haki uchaguzini, ambayo walinyimwa,” akasema.

Aliongeza kuwa hafla hiyo itatia nguvu Bunge la Mwananchi na kutoa mwongozo kwa mabunge ya kaunti kutatua kwa dharura changamoto za kiuchumi na kuhusu haki zinazokumba wananchi.

Mnamo Jumatatu, kamati andalizi ilisema maandalizi ya kumlisha Bw Odinga kiapo yamepiga hatua kubwa na kwamba maelezo zaidi yatatolewa baadaye.

Dkt Ndii alikamatwa Jumapili iliyopita akiwa Diani, Kaunti ya Kwale. Inadaiwa polisi waliomkamata kwa madai ya uchochezi walikuwa wanatafuta tarakilishi yake.