Ndani miaka 15 kwa ubakaji wa zamu

Na RICHARD MUNGUTI

Imepakiwa - Thursday, October 5  2017 at  15:27

Kwa Muhtasari

KIBARUA aliyeshtakiwa kwa ubakaji wa zamu Jumatano alisukumiwa kifungo cha miaka 15 bila faini. Alfred Otieno Oriwo atanyolewa bila maji kwa miaka hiyo 15 baada ya mahakama kusema “hafai kuishi na wapenda amani.”

 

Hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani Francis Andayi alisema mshtakiwa alimtendea unyama msichana huyo mwenye umri wa miaka 16 aliyemvumania akitoa kununua bidhaa dukani.

Kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Naulikha alimweleza hakimu kwamba mshtakiwa alikutana na mlalamishi kisha akamshika na kumpeleka katika jengo ambalo halikuwa limekamilika kujengwa na kumbaka kwa zamu akiwa na wavulana wengine.

“Lazima wenye tabia kama yako wajue kuna sheria inayowalinda wasichana na wanawake kwa jumla. Hupasi kumtia kumbaka msichana au mwanamke,” alisema Bw Andayi.

Hakimu alitupilia mbali ushahidi wa mshtakiwa kwamba  alikuwa na uhasama na jamii ya mlalamishi ndipo wakamwelekea.

“Ushhidi uliowasilisha ulithibitisha wewe ulimbaka mlalamishi baada ya kumweleza umekuwa ukimtamani kwa muda mrefu,” alisema Bw Andayi.

Mshtakiwa aliamriwa awe akifanyakazi ngumu gerezani ndipo iwe funzo kwa wengine wenye tabia kama yake.