http://www.swahilihub.com/image/view/-/4180468/medRes/1805356/-/14l0rka/-/al.jpg

 

Nilishinda kutokana na umaarufu wangu, sikumhonga yeyote - Duale

Wakili Ahmednassir Abdullahi (kulia) anayemwakilisha Aden Duale akimhoji Dkt Noah Akala, mtaalamu wa teknolojia ya KIEMS, Novemba 9, 2017. Picha/RICHARD MUNGUTI 

Na RICHARD MUNGUTI

Imepakiwa - Thursday, December 7  2017 at  15:46

Kwa Muhtasari

MBUNGE wa Garissa mjini Aden Duale aliambia mahakama ya kusikiza kesi za uchaguzi kwamba, uchaguzi uliopita ulikuwa shwari na alimshinda mpinzani wake Farah Maalim kutokana na umaarufu wake na wala sio kuwahonga wapiga kura.

 

Bw Duale ambaye pia ni kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa alikanusha kwamba, watu kutoka jamii nyingine walitishwa na kuhama eneo hilo kusudi wasishiriki katika uchaguzi mkuu.

Mbunge huyo alisema eneo la Garissa lina mkusanyiko wa jamii nyingi na kwamba, hakuna watu kutoka jamii yoyote “waliopokea vitisho kwa lengo la kuwazuia kushiriki katika uchaguzi mkuu uliopita.”

Alimweleza Jaji Hedwig Ong’udi kwamba, alimshinda Bw Maalim kwa njia halali.

Bw Maalim aliwania kiti hicho cha ubunge kwa tikiti ya chama cha Wiper Democratic Movement.

“Baada ya kura kuhesabiwa nilipata kura 21,300 naye Bw Maalim aliyekuwa naibu wa zamani wa Spika katika bunge la kitaifa alizoa kura 14, 745,” alisema Bw Duale.

Bw Duale aliyewania kiti cha Garissa Mjini kwa tikiti ya Chama cha Jubilee alisema alipata asilimia 54 ya kura zilizopigwa katika eneo hilo.

“Katika maeneo yote ya sehemu hii ya uwakilishi bungeni, umaarufu wangu ni zaidi ya asilimia 95 ndipo nikaweza kumshinda mpinzani wangu,” alisema Bw Duale.

Akijitetea dhidi ya madai kwamba alitumia ukora kutwaa ushindi katika uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017, Bw Duale alisema alifuata sheria za uchaguzi na kuzitii kikamilifu. Bw Duale alimfahamisha Jaji Hedwig Ong’udi kwamba uchaguzi katika eneo lote la Garissa mjini uliendeshwa kwa njia ya amani na wala hakukuwa na visa vyovyote vya ghasia kama ilivyodaiwa.

Alikanusha madai kwambaa maafisa wa tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) walitoka katika ukoo wake.

Alisema IEBC iliwaajiri makarani kulingana na kuhitimu kwao na wala hakuhusika kwa njia yoyote ya kuwateua walioendeleza uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017.

Bw Duale alisema kwamba baada ya shughuli za kuhesabu kura kukamilika alikabidhiwa cheti cha ushindi mwendo wa saa nne usiku.

“Hakukuwa na mwaniaji kiti mwingine katika ukumbi wa kuhesabia kura nilipokabidhiwa cheti cha ushindi,” alisema Bw Duale.

Alikanusha madai kwamba alishawishi IEBC kumhamisha afisa aliyekuwa anasimamia uchaguzi huo kumpeleka kwingineko ndipo zoezi hilo lisimamiwe na afisa ambaye angelimsaidia kushinda kiti hicho.

Kesi itaendelea Januari 8, 2018.