http://www.swahilihub.com/image/view/-/4260290/medRes/1856575/-/6yjm0r/-/NGILUU.jpg

 

Nilishinda kutokana na uzoefu wangu kisiasa na utendakazi mwema - Ngilu

Gavana Charity Ngilu akitoa ushahidi katika mahakama kuu Alhamisi katika kesi aliyoshtakiwa na Dkt Julius Malombe aliyeshindwa katika uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017. Picha/ RICHARD MUNGUTI 

Na RICHARD MUNGUTI

Imepakiwa - Thursday, January 11  2018 at  17:14

Kwa Muhtasari

GAVANA Charity Ngilu aliambia mahakama kuu Alhamisi kwamba ukwasi wake wa siasa wa robo karne ndio ulimwezesha kuwaangusha miamba wa siasa waliojitosa ulingoni kung’ang’ania ugavana wa Kitui mnamo Agosti 8, 2017.

 

“Wakazi wa Kitui waliamua kunichagua sio kwa misingi ya kijinsia mbali ni kwa vile wanajua utenda kazi wangu.

Wanajua historia yangu kama Kiongozi wa miaka 25 nilipokuwa Waziri katika wizara mbalimbali katika Serikali ya rais mstaafu Mwai Kibaki na nilipokuwa Waziri wa Ardhi katika Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta,” alisema Bi Ngilu akihojiwa na wakili Elias Masika wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC.

Gavana Ngilu alimweleza Jaji Pauline Nyamweya kwamba uchaguzi mkuu wa 2017 ulikuwa na ushindani mkali lakini “aliwapiku wapinzani wake kutokana na ukwasi wake wa siasa na namna alivyowatumikia wananchi wa kaunti hiyo siku za hapo awali.”

“Rekodi yangu ya maendeleo ndiyo nguvu yangu,” aliambia mahakama

Mwanasiasa huyo ambaye 1992 aliwania kiti cha Urais na kushindwa na rais mstaafu Bw Daniel arap Moi alisema anaelewa sheria za uchaguzi na kwamba madai aliwahonga na kuwatisha wapiga kura ni mihemko ya watu waoga.

Dkt Malombe aliyewasilisha kesi kupinga ushindi wa Bi Ngilu aliibuka wa tatu kwa kuzoa kura 74,000 ilhali aliyekuwa Seneta David Musila alipata kura 115,000 naye Bi Ngilu akazoa kura 169,000.

“Mlalamishi alikuwa ameshindwa na Bi Ngilu kwa zaidi ya kura 94,000,” wakili Kioko Kilukumi anayemwakilisha Bi Ngilu alisema.

Bi Ngilu alikanusha madai aliwahonga wapiga kura na kusema maajenti wa wapinzani wake ndio waliokamatwa  na kushtakiwa kwa kuwahoga wapiga kura.

Bi Ngilu alimsihi Jaji Nyamweya atupilie mbali kesi hiyo ya kupinga ushindi wake ndipo awahudumie wakazi wa kaunti ya Kitui kama alivyowaahidi bila bughudha.