http://www.swahilihub.com/image/view/-/4801284/medRes/2137557/-/a5g0v7/-/wife.jpg

 

Oparanya: Siasa zinakwamisha kilimo cha miwa

Gavana wa Kakamega, Wycliffe Oparanya  

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Thursday, October 11  2018 at  14:02

Kwa Muhtasari

Serikali haitasita kuadhibu kisheria viongozi wanaokandamiza wakulima

 

Kisumu. Wycliffe Oparanya ambaye ni gavana wa Kakamega amesema siasa ndizo zinakwamisha kilimo cha miwa.

Nyanza na Magharibi mwa Kenya ndiyo maeneo yanayojulikana kwa ukuzaji wa miwa. Akihutubu Alhamisi mjini Kisumu katika mkutano uliowaleta pamoja viongozi kutoka Nyanza na Magharibi, ili kujadili mwelekeo wa kilimo cha miwa, gavana huyu alisema ukuzaji wa zao hili utaimarika iwapo siasa zitakosa kuingizwa.

Oparanya alieleza kusikitishwa kwake na masaibu yanayowafika wakulima wa miwa, hasa soko duni, kukosa kulipwa mazao yao na kuwepo kwa sukari bandia nchini, hatua iliyosababisha baadhi ya viwanda vya kusaga miwa kufungwa. Alisema shida zinazowafika zimetokana na kuingizwa kwa siasa kwenye masuala ya kilimo cha miwa.

"Iwapo una masuala ya binafsi au siasa, usiyaingize kwenye kilimo cha miwa. Kilimo cha miwa kinaendeshwa na zaidi ya wakulima milioni 10, kwa hivyo ukiingiza siasa unawaathiri moja kwa moja," alisema Oparanya akionekana kulenga viongozi wa maeneo hayo.

Gavana huyu alisema viongozi huchaguliwa na kuteuliwa ili kuwakilisha wananchi, hivyo basi ni wajibu wao kuhakikisha wanawatetea kwa vyovyote vile. Wakulima wa miwa wamekuwa wakilia sekta hiyo kudidimia kwa sababu ya kutolipwa kwa wakati ufaao na hata kukosa kulipwa kabisa.

Viongozi wa viwanda vya sukari pamoja na wanasiasa wananyooshewa kidole cha lawama, wengine wakifuja pesa zinazofaa kulipwa wakulima. Katika ufunguzi wa maonyesho ya kilimo (LSK) 2018 jijini Nairobi wiki iliyopita, Rais Uhuru Kenyatta alionya kuwa serikali yake haitasita kuadhibu kisheria viongozi wanaokandamiza wakulima kwa kukosa kuwalipa mazao yao.

Alisema ni haki kwa kila mkulima kulipwa mazao yake iwapo ameyauzia kwa bodi husika. Mawakala pia ni kero kuu kwa wakulima nchini, ambapo hununua mazao yao kwa bei duni.