Ouda aapa kumshtaki Boinnet kwa kuwa 'polisi waliwapiga risasi waandamanaji'

Fred Ouda

Mbunge wa Kisumu ya Kati Fred Ouda akihutubia wanahabari katika majengo ya Bunge, Nairobi Oktoba 12, 2017. Picha/ CHARLES WASONGA 

Na CHARLES WASONGA

Imepakiwa - Thursday, October 12  2017 at  20:58

Kwa Mukhtasari

MBUNGE wa Kisumu ya Kati Fred Ouda ameapa kumshtaki Inspekta Mkuu wa Polisi Joseph Boinnet kufuatia tukio ambapo polisi waliwapiga risasi na kuwajeruhi waandamanaji mjini Kisumu Jumatano.

 

Akiongea na wahabari Alhamisi katika majengo ya bunge, Nairobi, Bw Ouda vile vile aliitaka Mamlaka Huru ya Kutathmini Utendakazi wa Polisi  (IPOA) kuchunguza kisa hicho ambapo takriba watu 27 walipata majeraha ya risasi na kulazwa hospitalini.

"Ninataka kusema hapa wazi wazi kwamba mimi kama Mbunge wa Kisumu ya Kati nitawasilisha kesi mahakama kumshtaki Inspekta Jenerali wa Polisi Joseph Boinnet kufuatia kisa ambapo watu wangu walipigwa risasi na kujeruhiwa na wakitekeleza haki yao ya kikatiba ya kuandama. Nachukua hatua hiyo kwa sababu polisi hao walipa maagizo kutoka kwa Mkuu wao ambaye ni Boinnet," akasema.

Hata hivyo, Mbunge huyo hakusema ni lini ataenda mahakamani kuwasilisha kesi hiyo.

Kisa hicho kilitendekea katika mtaa wa Kondele, ulioko katika eneo bunge analoliwakilishja Bw Ouda. Waliojeruhi wamelazwa katika hospitali mbalimbali ikiwemo ile ya Mafunzo na Rufaa ya Oginga Odinga ambako wanatibiwa majeraha ambayo madaktari wanasema ni ya risasi.

Wakati huo huo Bw Ouda amemkashifu Waziri wa Usalama Fred Matiang'i kuatia hatua yake ya kuzima maandamano katika miji ya Nairobi, Kisumu na Mombasa.

Kulingana naye Serikali inapasa kudumisha usalama wakati wa maandamano na kupambana na wahalifu wenye nia mbaya ya kupora na kuharibu mali.

"Nawalaani wahalifu wachache ambao hupora mali na kuwahangaisha watu wakati wa maandamano na kuitaka serikali kupambana nao.

Lakini hii sio sababu tosha kwa Waziri Matiang'i kuzima maandamano ambayo ni haki ya kikatiba ya raia," akasema huku akitoa wito kwa wafuasi wa NASA katika miji hiyo kuendelea kushiriki maandamano kushinikiza mageuzi katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).