Pasta pabaya kwa kuahidi miujiza hewa

Na ORNELIUS MUTISYA

Imepakiwa - Tuesday, November 28  2017 at  17:41

Kwa Muhtasari

KATHIANI MJINI

WAUMINI wa kanisa moja mjini hapa walizua kasheshe walipomzomea pasta wao peupe baada ya miujiza aliyokuwa amewaahidi kukosa kutimia!

 

Kulingana na mdokezi, pasta aliwaambia waumini waliokuwa na mahitaji mbalimbali wajitokeze mbele ya madhabahu ili awaombee. Aliwaahidi kuwa watapata miujiza baada ya muda wa siku tisini.

“Nimepata maono kutoka kwa Mungu kwamba baada ya muda wa siku tisini, kila mmoja wenu atakuwa na ploti yake mjini hapa,” pasta aliahidi waumini wake.

Inasemekana kwamba waumini hao walijawa na furaha ghaya na asilimia kubwa wakajipanga foleni mbele ya madhabahu waombewe ili wapokee miujiza hiyo.

“Mtu wa Mungu alimtaka kila mmoja apande mbegu ili apate miujiza iliyokuwa njiani yaja,’’ alieleza mdaku wetu.
Penyenye za mtaa zaarifu kuwa, siku tisini zilipita na utabiri wa pasta ukadhihirika kuwa mzaha.

Waumini walipandwa na hasira za mkizi na wakaapa kumkabili awarejeshee hela walizopanda mbegu la sivyo, wamuonyeshe cha mtema kuni.

Siku ya tukio, waumini walifika kanisani mapema kuliko siku zingine na wakakaa kwa utulivu mwingi. Ibada iliendelea kama kawaida hadi wasaa wa kutoa sadaka ulipowadia na kwa kauli moja wakakataa kutoa matoleo yao

Duru zaarifu muumini mmoja alinyanyuka kwa ghadhabu na akamtaka pasta awarejeshee hela alizowalaghai akiwaahidi miujiza hewa. Waumini kadha waliingilia na kuzua purukushani humo kanisani.

“Kanisa liligeuka ulingo wa masumbwi huku baadhi ya waumini wakimtetea pasta,’’ alisema mdokezi wetu.
Penyenye zaarifu kuwa pasta aliwaambia baraka kutoka kwa Mungu huja polepole na hivyo hawakuwa na budi ila kuwa na subira. “Kanisa hilo liligawanyika kutoka siku hiyo,” alisema mdokezi.