Polisi achunguzwa kwa hukahangaisha mshukiwa kimapenzi

Na ERIC MATARA

Imepakiwa - Thursday, December 7  2017 at  15:43

Kwa Muhtasari

AFISA wa polisi katika kituo cha polisi cha Mwariki, mjini Nakuru, amehusishwa na kisa cha kumdhulumu kingono mwanamke mchanga mwenye umri wa miaka 19 aliyezuiliwa katika kituo hicho.

 

Polisi wamesema wanachunguza madai kuwa afisa huyo alimhangaisha mwanamke huyo akitaka kushiriki naye mapenzi ndipo awachiliwe huru.

Kulingana na Bw Nelson Gitonga, mlezi wa mwanamke huyo yatima, mwathiriwa alikamatwa Jumatatu kwa madai ya kupatikana akiwa mlevi saa zisizofaa.

“Alikuwa na rafiki wakielekea kwa mazishi ya jamaa yao alipokamatwa. Nilipata habari kutoka kwa rafiki yake baadaye kuwa alikuwa akizuiliwa katika kituo cha polisi cha Mwariki,” akaeleza.

Tukio hilo liliwekwa mitandao ya kijamii na mwanaharakati fulani na watu wengi wakataka mshukiwa akamatwe mara moja.

Afisa mkuu wa polisi Nakuru, Bw Joshua Omukata alisema uchunguzi umeanza.