Raia wa Uganda aliyetoweka sasa asakwa

Na BENSON MATHEKA 

Imepakiwa - Monday, March 20   2017 at  14:34

Kwa Mukhtasari

RAIA wa Uganda aliyeshtakiwa kwa kumlaghai mtalii kutoka Jordan zaidi ya Sh16 milioni akidai angemuuzia kilo 50 za dhahabu, anasakwa na polisi baada ya kutoweka. 

 

Upande wa mashtaka uliambia mahakama kwamba Twahir Ismail huenda aliondoka nchini na polisi watatumia polisi wa kimataifa kumsaka. 

"Kuna habari kwamba mshtakiwa aliondoka Kenya baada ya kuachiliwa kwa dhamana na polisi wanawasiliana na vitengo vingine kumsaka, "kiongozi wa mashtaka Zafida Chege aliambia mahakama.

Alisema mshtakiwa hakuwa raia wa Kenya na polisi wanafanya kila juhudi kumkamata. Bw Twahir Ismail 36, ameshtakiwa kwa kupokea pesa hizo kutoka kwa Mohammed Mozyed Hassan Bataineh akimwambia kwamba alikuwa mfanyabiashara wa kuuza dhahabu.

Kulingana na shtaka, ilidaiwa kwamba Ismail alitenda kosa hilo katika kati ya Aprili 17 na Juni 15, 2015 katika barabara ya Kabeserian mtaani Lavington Nairobi akijua kwamba alikuwa akimlaghai Bw Mohammed.

Kwenye shtaka la pili ilidaiwa kwamba alipatikana nchini kinyume cha sheria akiwa raia wa Uganda.

Kulingana na shtaka, Ismail hakuwa na kibali cha kumruhusu kuishi nchini alipokamatwa na maafisa wa polisi. 

Wakati aliposhtakiwa upande wa mashtaka ulieleza Hakimu Mkuu wa Kibera  kwamba mshtakiwa alikuwa na kesi katika mahakama nyingine nchini iliyotwaa paspoti yake ili asitoroke.

Hakimu Mkuu Joyce Gandani aliagiza polisi waendelee kumsaka na kumfikisha korti. "Nimewapa kibali cha kumkamata. Fanyeni kila juhudi," alisema. Kesi itatajwa Mei 8 mwaka huu.