http://www.swahilihub.com/image/view/-/1593896/medRes/359833/-/vgi8j0z/-/DnAG1704a.jpg

 

Raila aonywa dhidi ya kuapishwa Desemba 12

Githu Muigai

Mwanasheria Mkuu Prof Githu Muigai. Picha/MAKTABA 

Na B. MUTANU na S. KIMATU

Imepakiwa - Thursday, December 7  2017 at  18:23

Kwa Muhtasari

MWANASHERIA Mkuu Prof Githu Muigai amemuonya kinara wa muungano wa NASA, Raila Odinga, dhidi ya kuapishwa Desemba 12, akitaja kitendi hicho kuwa hatia ya uhaini ambayo hukumu yake ni kunyongwa.

 

Profesa Muigai alisema Alhamisi kuwa kuapishwa kwa Bw Odinga ni kinyume cha sheria, haramu na batili.

“Hatujapokea taarifa yoyote kuhusu kuapishwa kwa viongozi wa upinzani na hatuwezi kukubali ilani ya kitendo cha uhaini. Adhabu ya kitendo hicho ni kunyongwa,” Profesa Muigai akaambia wanahabari afisini mwake jijini Nairobi.

Alisema Kenya inaongozwa chini ya katiba na sheria na kwamba hakuna mtuanayeweza kudai au kutekeleza mamlaka ya kitaifa kama hajakubaliwa kikatiba.

“Jaribio lolote la kumwapisha mtu yeyote kama rais, isipokuwa tu aliyechaguliwa kwa mujibu wa katiba na kwa kufuata utaratibu unaofaa, ni kinyume cha sheria,” akasema Profesa Muigai.

Alifafanua kuwa katiba inasema ni lazima rais aapishwe na Jaji Mkuu baada ya kutangazwa mshindi na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutokana na uchaguzi na akaonya kuwa watu wote watakaoshiriki katika hafla hiyo (iwapo itafanywa) wataadhibiwa kisheria.

Muungano wa NASA umesisitiza kuwa haumtambui Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto na umeapa kumwapisha Bw Odinga siku ya Jamhuri, Desemba 12.

Jana, Askofu Mkuu wa Kanisa la Oasis of Grace Churches, Bw George Kamunya, alionya kuwa kumuapisha Bw Odinga kunaweza kuzua ujo.

Maafa

“Kumuapisha Raila kutaleta vurugu na huenda tukashuhudia maafa nchini. Hili ni jambo ambalo taifa lolote haliwezi kulitaka,” akasema Bw Kamunya.

Profsa Muigai pia alitaja Mabunge ya Wananchi kuwa haramu akisema hayatambuliwi kikatiba.

“Dhana ya Mabunge ya Wananchi ni ngeni katika katiba. Haimo chini ya sheria inayosimamia serikali za kaunti wala sheria zingine,” akasema na kuongeza kuwa dhana hiyo ilikopwa kutoka kwa mashirika ya kijamii.

Kulingana naye, wananchi wanaweza kujisimamia kwa njia mbili pekee: Kwa kuchagua viongozi wao wakati wa uchaguzi, au kupitia kwa kura ya maamuzi.

Profesa Muigai alisema serikali ina uwezo wa kuadhibu kaunti zilizopitisha Mswada wa kuunda Mabunge ya Kaunti kwa kutoza viongozi wake malipo ya ziada kwa sababu walitumia pesa za umma kupitisha Miswada kinyume cha sheria.

“Hatua zozote za Mabunge ya Kaunti kupitisha Miswada ya kuundwa kwa Mabunge ya Wananchi ni haramu kwa sababu mabunge hayo hayana msingi wowote katika sheria tunazojua. Hayana wajibu wowote chini ya sheria za Kenya,” akasema.