http://www.swahilihub.com/image/view/-/4802514/medRes/2138287/-/22xh9w/-/odinga.jpg

 

Raila ataka ‘mashetani’ waadhibiwe vikali

Kiongozi wa ODM, Raila Odinga  

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Friday, October 12  2018 at  10:22

Kwa Muhtasari

Mauaji ya kikatili ya Sharon na Minica yamekuwa mjadala mkuu kwenye mitandao na vyombo vya habari

 

Murang'a, Kiambu. Kinara wa upinzani Raila Odinga jana alieleza kughadhabishwa kwake na kuongezeka kwa visa vya mauaji kwa wasichana.

Raila alisema ni jambo la kuhuzunisha taifa kuendelea kupoteza wasichana kupitia mauaji ya kikatili ambayo katika siku za hivi karibuni yamekuwa mjadala mkuu kwenye mitandao na vyombo vya habari. Alitaja mauaji ya kinyama ya Monica Kimani na Sharon Otieno kama yasiyofaa kukubalika katika jamii.

"Wanaowashika na kuua wasichana wadogo ni mashetani (akimaanisha wamekosa utu)," alisema Raila. Kiongozi huyu wa Orange Democratic Movement (ODM) alikuwa akiongea katika hafla ya mazishi ya mwanamuziki wa nyimbo za Agikuyu, Joseph Kamaru, katika kaunti ndogo ya Kigumo, Murang'a.

Aidha, Raila alisifu msanii huyo ambaye hadi kufariki kwake alikuwa na zaidi ya nyimbo 3,000, akieleza kwamba alitumia talanta yake kukemea maovu kama mauaji kwa wasichana.

"Wasichana hawapigwi wala kutendewa unyama kama tunaoshuhudia. Ninashangazwa na watu wenye akili timamu wakimkata msichana shingo na mjamzito kudungwa kisu pamoja na kijusi, haya ndiyo maovu Joseph Kamaru alikashifu," alieleza.

Raila alipendekeza watakaopatikana na hatia katika kuhusika kwa mauaji ya Sharon na Monica waadhibiwe vikali.

Monica alipatikana ameuawa mnamo Septemba 20, 2018 kwenye nyumba yake katika mtaa wa kifahari wa Kilimani, jijini Nairobi. Alizikwa nyumbani kwao Gilgil, kaunti ya Nakuru. Washukiwa wa mauaji ya msichana huyo ni mtangazaji Jacque Maribe na mpenzi wake, Joseph Irungu maarufu kama Jowie, ambao wangali rumande wakisubiri kufunguliwa mashtaka kwa mujibu wa amri ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma (DPP) Noordin Haji. Jumatatu wiki hii Haji aliamuru wafikishwe katika mahakama kuu kufunguliwa mashtaka akisema ana ushahidi wa kutosha.

Washukiwa wakuu katika mauaji ya Sharon Otieno, aliyekuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Rongo ni gavana wa Migori Okoth Obado, msaidizi wake wa karibu Michael Oyamo na Caspel Obiero, karani katika serikali ya kaunti ya Migori. Watatu hao wangali kizuizini.

Inasemekana Sharon alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na gavana Obado. Mwanafunzi huyo alitykuwa na miaka 26, alikuwa na ujauzito wa miezi saba na alitekwa nyara Septemba 3 mwaka huu, kisha akapatikana ameuawa Septemba 5 katika msitu mmoja Homa Bay katika hali isiyoeleweka.