Tutahakikisha Raila hatashinda urais - Wabunge wa Jubilee

Moses Kuria

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria. Picha/MAKTABA 

Na ALEX NJERU

Imepakiwa - Monday, June 19   2017 at  07:43

Kwa Mukhtasari

WABUNGE kadhaa wa chama cha Jubilee wameapa kwamba watahakikisha mgombeaji urais wa muungano wa NASA Raila Odinga hatatawala Kenya.

 

Wakihutubia wakazi wa Tharaka- Nithi mjini Chuka Jumamosi wakiwa kwenye msafara wa Mbele Kuko Sawa kupigia debe Rais Uhuru Kenyatta, wabunge Moses Kuria (Gatundu), Muthomi Njuki (Chuka/Igambang’ombe) na mwakilishi wa wanawake kaunti ya Tharaka -Nithi Beatrice Nkatha, walisema watafanya kila wawezalo kuhakikisha Raila hataongoza Kenya.

Walimfananisha Raila na baba yake, Jaramogi Oginga Odinga wakisema jinsi alivyokosa kuwa rais, mwanawe (Raila) pia hatakuwa rais wa Kenya.

“Tunataka kumwambia Bw Odinga kwamba ndoto yake ya kuongoza nchi hii haitatimia na anapasa kustaafu siasa,” alisema Bw Kuria.

Wabunge hao waliotembelea maeneo tofauti kaunti hiyo kumpigia debe Rais Kenyatta kuchaguliwa kwa kipindi cha pili walisema Bw Odinga hana uwezo wa kuongoza nchi.

Bw Kuria alisema Bw Odinga hana ajenda yoyote ya kuwafaa Wakenya isipokuwa kuzunguka akiburudisha watu na kukosoa serikali.

Kuhujumu uchaguzi

Mbunge huyo mbishani alidai kwamba Bw Odinga hataki uchaguzi na anapanga kuhujumu mipango ya uchaguzi mkuu ujao ili kushinikiza muungano wa NASA kushirikishwa katika serikali ya muungano ilivyotendeka baada ya uchaguzi mkuu wa 2007.

Bw Kuria alisema Jubilee haitakubali ushawishi wowote wa jamii ya kimataifa Bw Odinga kugawana mamlaka na Rais Kenyatta.

Bw Njuki alikosoa NASA kwa kumhusisha Rais na familia yake na tenda ya kuchapisha karatasi za kura iliyopatiwa kampuni ya Al Ghurair akisema ni njama za kuvuruga maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8.

“Hata Bw Odinga akipatiwa nafasi ya kuchapisha karatasi za kura hawezi kumshinda Bw Kenyatta,” alisema Bw Njuki.

Bi Nkatha alisema ziara ya viongozi wa NASA katika eneo la Mlima Kenya haitabadilisha wapigakura.

“Eneo hili litabaki kuwa ngome ya Jubilee,” alisema Bi Nkatha.

Viongozi wa NASA waliandaa mikutano kadhaa katika kaunti za Tharaka Nithi na Meru ambayo ilivutia watu wengi.